Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa Sugar yaaga rasmi Ligi Kuu Bara

Mtibwa Washuka Mtibwa Sugar yaaga rasmi Ligi Kuu Bara

Sat, 25 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabingwa wa zamani wa Tanzania msimu wa 1999 na 2000, Mtibwa Sugar imeshuka rasmi jana baada ya kufumuliwa mabao 3-2 na Mashujaa katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Mtibwa iliyoanzishwa mwaka 1988 na kupanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) 1996, imeshuka kutokana na kusaliwa na pointi 21 ikiwa na mechi moja mkononi ambayo hata ikishinda haiwezi kuiokoa kwani tayari pointi hizo zimeshapitwa na timu nyingine zilizopo juu yake.

Kanuni za Ligi Kuu ni kwamba, timu zinazoshika nafasi mbili za mwisho zinashuka moja kwa moja na zile zinazomaliza nafasi ya 13 na 14 zinacheza mchujo (play-off) zenyewe kwa zenyewe na mshindi husalia katika ligi hiyo na ile inayopoteza inacheza na mshindi wa mechi kama hizo kwa timu za Ligi ya Championship.

Mabao yaliyoizamisha Mtibwa iliyokwenda Kigoma bila Kocha Mkuu, Zubeiry Katwila na yule wa makipa, Patrick Mwangata pamoja na meneja wa timu Henry Joseph na kuachiwa kocha msaidizi, Awadh Juma, yaliwekwa kambani na Reliant Lusajo aliyefunga mawili dakika ya tatu na 26 na lile la Mundhir Vuai la dakika ya 32.

Mtibwa ilipata mabao ya kufutia machozi kupitia kwa Rashid Seif Karihe aliyefunga katika dakika ya 15 na Samson Madekele alijifunga katika harakati za kuokoa dakika ya 55.

Ushindi huo umetoa nafuu kwa Mashujaa kwani imefikisha pointi 32 ikiwa nafasi ya 11 na sasa inasikilizia mchezo wa mwisho dhidi ya Dodoma Jiji ukitarajiwa kupigwa Jumanne kwenye uwanja wa nyumbani, Kigoma na iwapo itaibuka na ushindi itasalimika hata kucheza play-off.

Mtibwa sasa inasubiri kukamilisha ratiba Jumanne ugenini kucheza na Ihefu ambayo leo imeicharazwa mabao 2-0 na Dodoma Jiji katika pambano lililopigwa Uwanja wa Liti, mjini Singida.

Chanzo: Mwanaspoti