Nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika na Small Simba, Simba na Mtibwa Sugar, Dua Said amekiangalia kikosi cha sasa cha Wakata Miwa wa Manungu na kuwapa mchongo wa maana wa kuisaidia kurejesha makali yao kama ilivyokuwa zamani kisi cha kubeba taji la Ligi Kuu mara mbili.
Dua aliliambia Mwanaspoti, ili timu iweze kufanya vizuri ni lazima ifanye usajili mzuri kitu ambacho kwa sasa Mtibwa imekuwa ikichemka tofauti na enzi za nyuma akiitaka iklichuana na Tanzania Prisons na sio Simba na Yanga ambazo wao walizichukulia za kawaida na kuzifunika kwenye ligi.
"Usajili mzuri uliofanywa kipindi hicho na maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa msimu yaliibeba timu. Nakumbuka timu iliyokuwa inatusumbua ni Prisons, kwani ilikuwa fiti, ila hizi Simba na Yanga wala hazikusumbua kipindi hicho Mtibwa ikiwa Mtibwa kweli," alisema Dua aliyewahi kucheza soka la kulipwa Uarabuni.
Mkongwe huyo alisema kwa sasa Mtibwa inasumbuliwa na kukosa viungo bora kutokana na usajili wao kuwa chini na anaishauri kwa kuwaambia haiwezi kufanya vizuri kwa kutegemea wachezaji wengi vijana na badala yake wafanya usajili wa maana ukihusisha wazoefu ili mambo yawe mazuri.
"Pesa inaweza kuwa ni tatizo la kutokufanya usajili mkubwa, lakini wawe na uhakika watakaposajili tu lazima watapata matokeo mazuri yatakayowavutia hata wawekezaji kuja na hapo ndipo wataona faida za kuwekeza kwao kwenye usajili," alisema Dua.
Mtibwa ilitawala soka mara ilipopanda miaka ya mwisho ya 1990 na kubeba taji mara mbili mfululizo 1999 na 2000 kabla ya kupoteza kiasi cha kupambana kuepuka kushuka daraja mara kadhaa ikiwamo msimu uliopita iliponusurika kupitia mechi za play-off kwa kuifunga Tanzania Prisons.
Baadhi ya wachezaji walioibeba Mtibwa enzi hizo ni pamoja na Kassim Issa, Salhina Mjengwa, Thomas Masamaki, Geofrey Magori, Salum Mayanga, Mecky Maxime, Moja Liseki, Yusuph Macho, Steven Nemes, Zubeiry Katwila, chini ya kocha John Simkoko na uratibu wa timu hiyo Jamal Bayser.
Timu hiyo mapema wiki hii ilifumuliwa mabao 2-0 na Azam na kung'olewa katika robo fainali ya Kombe la ASFC, taji ililowahi kulibeba mwaka 2018 kwa kuifunga Singida United katika fainali zilizopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.