Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa Sugar kama wameamua hivi

Mtibwa Ligi Kuu Mtibwa Sugar kama wameamua hivi

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tunajisahau na usajili unaofanywa na timu za Ligi Kuu Bara lakini huko katika Ligi ya Championship kuna watu wanajipanga hasa kuhakikisha wamo kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Miongoni mwa timu za Championship zinazofanya usajili wa kibabe ni Wakata Miwa wa Mtibwa Sugar ambao msimu uliopita wa 2023/2024 waliaga Ligi Kuu baada ya kushika mkia katika msimamo wakati msimu ulipofikia tamati.

Ni kama jamaa waling’atwa na nyoka na sasa wanashtuka kutokana na maingizo ya watu stahiki katika timu yao wanayofanya hivi sasa kabla ya kuanza kwa pilika za ligi yao ambayo hapo nyuma ilijulikana kama Ligi Daraja la Kwanza.

Kwanza walimrudisha kundini Abubakar Swabr na kumpa nafasi ambayo alihudumu hadi alipoachana na klabu hiyo mwaka uliopita ya mtendaji mkuu.

Huyu analifahamu vyema soka la Tanzania na mahitaji yake, hivyo atakuwa kiungo muhimu baina ya timu hiyo na viongozi wa kiwanda cha Mtibwa wanayoimiliki timu hiyo, lakini mtekelezaji na msimamizi sahihi wa mipango ambayo utawala wa timu hiyo umepanga.

Kwa kuanza, amemshusha kocha wa daraja la juu, Melis Medo kwa ajili ya kuinoa timu hiyo jambo ambalo litawatengeneza kisaikolojia wachezaji waone kuwa wao sio timu ya kucheza Championship na badala yake wanatakiwa kuwepo Ligi Kuu.

Baada ya hapo imefanya usajili wa haraka wa wachezaji watatu ambao sio tu wana uzoefu wa soka la Tanzania bali pia wamecheza Ligi Kuu katika timu tofauti ambao ni Anuary Jabir, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Amani Kyata.

Wanaitengeneza timu yao kuwa na mtazamo wa Ligi Kuu, huku ikiwa Ligi ya Championship jambo ambalo bila shaka litaongeza morali na ari kwa timu yao kwani wachezaji watajiona wana deni la kulipa kwa uongozi wa timu hiyo.

Kitendo cha kuwa na makocha na wachezaji wa hadhi ya ligi kuu kinaashiria pia jamaa wamejipanga vilivyo kwenye suala zima la kiuchumi ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kuamua timu za kupanda kutoka Championship kwenda Ligi Kuu Bara.

Chanzo: Mwanaspoti