Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa, Prisons rekodi zitaamua

Prisons Vs Mtibwa Mtibwa, Prisons rekodi zitaamua

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara inarejea baada ya kupisha mechi za michuano ya ASFC, kwa mabingwa wa zamani Mtibwa Sugar kuwa wageni wa Tanzania Prisons, huku rekodi zikitarajiwa kuamua pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini hapa.

Huo ni mchezo wa pili kwa wataka miwa hao, kwani mechi iliyopita ilivaana na Mbeya City na kulala 1-0, huku rekodi ikiongeza timu hiyo imeshinda mara ya mwisho Novemba 21 ilipoilaza Polisi Tanzania, kitu kinachoifanya leo igangamale mbele ya maafande wa Prisons.

Mbali na kutoshinda tangu Novemba, lakini Mtibwa imechezea mechi 10 ugenini bila kutokana na ushindi, huku kwa sasa ikiwa na pointi 25 katika nafasi ya nane na sare ya mwisho kupata ugenini ilikuwa dhidi ya Ruvu Shooting, Desemba 20 mwaka jana.

Mabingwa hao wa TPL 1999 na 2000 imekuwa njema zaidi nyumbani ambapo katika michezo 11 imeshinda michezo mitano, sare nne na kupoteza michezo miwili dhidi ya Yanga (1-0) kisha ikalala mbele ya Azam kwa kichapo cha mabao 4-3.

Msimu uliopita timu hizi zilinusurika kusuka daraja baada ya kumaliza msimu, Mtibwa ikiwa nafasi ya 13 kwa alama 31 huku Prisons nafasi ya 14 kwa alama 29 na kukutana hatua ya mtoano.

Katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Sokoine, Prisons ikafa 3-1 na mchezo wa marudiano ikashinda 1-0 na kuifanya Mtibwa kubaki huku Prisons ikienda kujitetea mbele ya JKT Tanzania iliyokuwa ikiwania kupanda Ligi Kuu lakini bahati ikaiangukia Prisons.

Kuanzia mwaka 2015 zimekutana kwenye Ligi Kuu mara 15, Mtibwa ikishinda mara tatu na mara zote ikiwa nyumbani huku sare ikiwa michezo tisa na ikipoteza michezo mitatu.

Kocha wa Mtibwa, Salum Mayanga alisema anatambua umuhimu na ugumu wa mchezo huo kutokana na mpinzani wanayekwenda kukutana naye ambao kwa sasa inanolewa na Abdallah Mohammed 'Baresi'.

Mayanga anakutana na Prisons timu ambayo alidumu nayo kwa misimu miwili lakini Desemba 12, 2021, alitangaza kuachana na timu hiyo akitimkia Mtibwa Sugar aliyojiunga nayo Januari 7 mwaka huo akichukua nafasi ya Zubery Katwila aliyejiunga na Ihefu.

Akiwa Prisons, Mayanga alitangazwa kocha bora wa Ligi Kuu Novemba, 2021 huku mshambuliaji wa timu hiyo, Jeremiah Juma akiibuka mchezaji bora wa mwezi na baada ya kuondoka nafasi yake ikachukuliwa na Patrick Odhiambo.

Chanzo: Mwanaspoti