Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa, Mashujaa uzalendo wao unawaangusha

Ty Mashujaa Mtibwa, Mashujaa uzalendo wao unawaangusha

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hiki kinachotokea kwa Mtibwa Sugar na Mashujaa FC kwenye ligi msimu huu wala sio cha bahati mbaya na kiliandaliwa na wao wenyewe.

Achana na sababu nyingine zinazotajwa kuchangia timu hizo mbili kutofanya vizuri nimegundua iko moja kuu ambayo ndio inaziumiza kwa sasa.

Sababu hiyo ni usajili wa wachezaji wa daraja la kawaida wakati wa dirisha kubwa la usajili ambao umesababisha ugumu kwa makocha wao kutengeneza timu bora na za ushindani kupitia wachezaji hao.

Na hiyo imesababishwa na hali ya uzalendo ambayo Mtibwa Sugar na Mashujaa FC kila moja imekuwa nayo kwa ajili ya kutukuza vya nyumbani kwa kuamua kutosajili wachezaji kutoka nje ya nchi na badala yake kutoa fursa kwa wachezaji wa Kitanzania ili baadaye waje kusaidia timu za taifa.

Sasa bahati mbaya iliyozikuta timu hizo mbili ni kwamba hazikupata hao wazawa ambao wana daraja la juu zaidi la ubora wa kuziwezesha Mtibwa Sugar na Mashujaa FC kuleta ushindani mkubwa kwenye ligi ambao pengine ungezifanya zisiwe hapo zilipo leo hii.

Wazawa wenye kiwango cha juu zaidi iko wazi kwamba wapo katika timu tatu kubwa za Yanga, Simba na Azam na wale wanaowafuatia wakadakwa na timu nyingine ambazo angalau zilijitahidi kutenga dau nono la kuwashawishi wazitumikie na hivyo kuzifanya Mtibwa na Mashujaa kubakia na wale wa ziada.

Ukiwa na wachezaji kama hao hawatokupa muendelezo wa matokeo mazuri utalazimika kutumia muda mrefu kuwaunganisha pamoja hadi pale watakapoweza kuwa sawa, wakati huo wenzako ambao wana vikosi vizuri tayari wameshakuacha kwenye mataa.

Sera ya kusajili wazawa tu ni nzuri lakini timu inapaswa kuhakikisha kwamba wale wazawa bora zaidi ndani ya nchi inawapata na kuwahudumia vizuri ili waweze kuisaidia kupambana na zile ambazo zimejaza wageni jambo ambalo zitaziweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Vinginevyo kufanya uzalendo wa kuwapa fursa wazawa huku timu inawachukua wale wenye uwezo wa kawaida kunaleta athari kubwa kwenye timu mojawapo ndio kama hiyo ya kile kinachozikumba Mtibwa na Mashujaa.

Chanzo: Mwanaspoti