Kwenye Ligi Kuu Bara leo ni Mtibwa Sugar dhidi ya Dodoma Jiji, huku beki wa zamani wa Wakata Miwa wa Manungu anayekipiga Dodoma kwa sasa akitabiri utakuwa mchezo mgumu kwenye Uwanja wa Manungu Turiani.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, Mtibwa iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lilofungwa na mshambuliaji Charles Ilamfya, lakini Hassan Kessy aliyewahi kukipiga Mtibwa alisema ugumu wa mchezo huo unakuja kutokana na ubora wa wachezaji wa Mtibwa na benchi la ufundi.
Nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga alisema wamejipanga kupata matokeo ili kujiokoa na janga la kushuka daraja kwani timu hiyo imekuwa na matokeo yasiyoridhisha.
Nahodha wa Dodoma, Mbwana Kibacha alisema wapo tayari kwa mchezo huo na wanaamini watapata pointi tatu.
“Kila mmoja anajua ubora wa Mtibwa, utakuwa mchezo mgumu lakini ni lazima tupambane kuhakikisha tunapata matokeo,” alisema Kibacha.
Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Dodoma Jiji walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam mtanange uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Dodoma Jiji itawakosa,Jimmy Shoji na Christian Zigar kutokana na kuumia katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu Bara.