Achana na matokeo na nafasi yao kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Coastal Union ni moja ya timu ambazo zimekuwa zikiibua vipaji na kuvisambaza kwenye timu nyingine za Ligi Kuu zikiwamo, Yanga, Simba na Azam FC.
Mfano mzuri ni mabeki Bakari Mwamnyeto anayekipiga Yanga na ni nahodha wa timu hiyo, Abdallah Ame alisajiliwa na Simba sasa anakipiga KMC, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Ayoub Lyanga wote wapo Azam FC.
Haishangazi kuona Mwamnyeto akiwa tegemeo pia katika kikosi cha timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ na amedumu kutokana na kiwango bora alichoonyesha ndani ya muda mfupi.
Lyanga pia amekuwa akiitwa mara kwa mara ingawa amekuwa hana namba.
Coastal Union pamoja na kuondoa mastaa hao ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye timu zao mpya sasa imefanikiwa kutengeneza mastaa wengine ambao pia wanaonekana kuwa bora na ni suala la muda kuendelea kukaa ndani ya timu hiyo. Mmoja wao ni nahodha wa timu hiyo, kiungo Mtenje Albano.
Mwanaspoti limepata wasaha wa kufanya mahojiano na kiungo huyo fundi ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwamo kumtaja Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye kiungo wake bora na anajifunza mengi kutoka kwake.
ANAMTAZAMA FEI TOTO YOUTUBE
Anafunguka ubora wake kwa sasa ni kutokana na kujifunza na amekuwa akitumia mtandao wa You Tube kutazama maufundi kutoka kwa wachezaji anaowakubali, Fei Toto na Sergio Busquets wa Barcelona.
“Kila siku najifunza. Sitegemei mazoezi ya kocha pekee.”
“Natumia mitandao ya kijamii ‘You Tube’ kuangalia maufundi kutoka kwa wachezaji wengine ninaovutiwa nao ili kuongeza kitu. Pia nimekuwa nikitazama marudio ya mechi nilizocheza ili kubaini mapungufu na kuyarekebisha kabla ya mchezo mwingine.”
ANACHEZA NAFASI YOYOTE
Kiungo huyo anasema licha ya kutambulika zaidi akicheza nafasi ya kiungo, lakini ana uwezo wa kucheza nafasi yoyote uwanjani.
“Naweza kucheza nafasi yoyote. Ni kama askari aliye vitani, hawezi akakataa kisu akachagua panga. Anatumia silaha yoyote. Hivyo kocha akiamua kunipanga beki wa kati, nacheza kwa sababu ni kazi yangu.
“Nacheza kiungo mkabaji lakini muda mwingine kiungo mshambuliaji. Hii ndio maana halisi ya mchezaji na ndio maana natumika zaidi kwenye timu yangu tangu nimepandishwa. Naamini nina vitu vingi.”
MITINDO NAKO YUMO
Anasema soka ndio umempa ajira, lakini kama asingekuwa mchezaji, angekuwa mwanamitindo fani nyingine ambayo anaipenda ili kutangaza mitindo nje ya nchi.
“Kama si soka naamini ningekuwa mwanamitindo. Ni kitu kingine nakipenda zaidi ukiachana na soka ambao umenipa ajira Coastal.”
“Kucheza soka hakujakatisha ndoto yangu ya kuwa mwanamitindo. Ikitokea nikaamua kuachana na soka nitaibukia kwenye sanaa hiyo ya mitindo. Natamani kuwa bora kwenye sekta hiyo,” alisema kiungo huyo anayependa kuvaa na anatamani awe na mtu wa kumbunia mavazi.
ANAJUTA KISA BANGALA
Unakumbuka tukio la rafu mbaya aliyomchezea Yannick Bangala kwenye mchezo wa Ligi Kuu zilipokutana Coastal dhidi ya Yanga iliyoshinda mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Tukio hilo limekuwa likimtesa sana Mtenje licha ya kumwomba radhi beki huyo wa Mabingwa watetezi wa ligi kuu na mchezaji bora wa msimu uliopita.
“Najilaumu sana. Pamoja na kumwomba radhi, lakini limekuwa likinitesa hadi leo. Ukiniuliza kwa nini nilifanya vile, sikumbuki,” anasema na kuongeza;
“Matukio kama hayo huwa yanatokea. Huwa nayashuhudia kwa wenzangu na kujiuliza kwa nini wanafanya hivyo. Sasa nimefanya mimi. Sielewi ni kwa nini nilifanya hivyo. Baada ya mchezo niliongea naye pia nilifanya jitihada za kupiga simu kumwomba samahani na yeye alinihakikishia amenisamehe, lakini tukio hilo nimeliweka kwenye kumbukumbu zangu.”
KWA LYANGA AKILI TU
“Nimekutana na washambuliaji wengi lakini navutiwa zaidi na uchezaji wa Ayoub Lyanga anayekipiga Azam FC. Ni mchezaji anayetumia akili na sio nguvu. Hivyo nimekuwa nikikutana na changamoto inapofika nafasi yangu uwanjani kuhakikisha naipambania timu isipoteze mchezo,” anasema na kuongeza;
“Mbali na Lyanga pia kuna mshambuliaji wa zamani wa Geita Gold ambaye sasa amejiunga na Coastal Union, Juma Mahadh. Ni mchezaji ambaye amekuwa akinisumbua tukikutana kwenye mchezo wowote pamoja na kucheza nafasi ya kiungo, nimekuwa nikikutana nao na kunipa tabu.”
U20 HADI NAHODHA
Mtenje ambaye amekuwa na timu moja ‘Coastal’ kwa muda mrefu, anasema anafurahia maisha kwenye chama lake hilo la ‘Wagosi wa Kaya’ na anajivunia kuvaa kitambaa cha unahodha.
“Nimeitumikia timu hii kwa muda mrefu kuanzia timu ya vijana. Nafurahia maisha hapa kutokana na kuaminiwa na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Pia kupewa kitambaa cha unahodha. Ni heshima kubwa sana kwangu.”
MCHANGO WA MGUNDA, CHIPO
Anamtaja Kocha Juma Mgunda ndiye aliyemwamini na kumpa nafasi katika kikosi cha Coastal Union baada ya kumpandisha kutoka timu ya vijana na hawezi kusahau hilo.
“Nimepita chini ya makocha wengi, lakini Mgunda siwezi kumsahau. Aliniamini na kunipa nafasi moja kwa moja kikosi cha kwanza baada ya kupandishwa timu ya wakubwa,” anasema Mtenje na kuongeza hiyo imesaidia kwani kila kocha anayekuja amekuwa akijenga imani kwake akiwamo Kocha Yusuf Chipo ambaye anamshukuru pamoja na makocha wengine kwa kumwendeleza.