Mchezaji wa zamani wa Simba SC, Mtemi Ramadhani, ametuma ujumbe kwa viongozi wa klabu hiyo kwa kusema kama wanataka timu hiyo ifanye vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inabidi wasajili wachezaji bora.
Simba SC Ijumaa (Aprili 05) iliondolewa na Al Ahly katika Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa jumla ya mabao 3-0 kufuatia kufungwa mabao 2-0 ugenini wakati ikikubali 1-0 nyumbani.
Mtemi amesema uongozi wa Simba SC unatakiwa kufanya usajili wa wachezaji bora kuhakikisha inafanya vyema katika msimu ujao wa michuano ya kimataifa.
Amesema bado wachezaji wa Simba SC wana makosa madogo madogo ambayo yamekuwa yakifanyika kila wakati.
Mtemi amesema hata hivyo Simba SC inazidi kuimarika kufuatia kucheza michuano hiyo mara nyingi, lakini Al Ahly wana uzoefu mkubwa.
“Bado tunaendelea kujifunza, ninafikiri hii ni Robo Fainali ya nne au ya tano, kuna makosa madogo madogo ambayo yamekuwa yakifanyika, hivyo ninaamini kama uongozi ukifanya usajili mzuri, tutafanya vyema msimu ujao.
“Tusikate tamaa kwani timu inaendelea kupata uzoefu, hivyo tusikate tamaa kwani tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao,” amesema.
Simba SC ilifika katika hatua hiyo baada ya kuishia nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B kwa pointi tisa nyuma ya Asec Mimosas ya Ivory Coast ikiwa na pointi 12.