Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtego wa Yanga uko hapa

Yanga Warm Up Mbarali.jpeg Mtego wa Yanga uko hapa

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga SC imepoteza mechi moja tu katika Ligi Kuu Bara, huku ikiwa imeandika historia ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuikosa kwa miaka 25 iliyopita, sambamba na kupiga soka tamu linalokuna mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini.

Licha ya kushika nafasi ya tatu kwa sasa kutokana na kukusanya pointi 12 baada ya mechi tano za Ligi Kuu -- ikizidiwa na watani wao, Simba wenye pointi 15 na Azam iliyopo ya pili ikikusanya pointi 13 kila moja ikiwa imecheza pia michezo mitano -- Yanga imeonyesha kuwa na kikosi imara kikibebwa na nondo nne matata.

UKUTA WA CHUMA

Yanga ni moja ya timu iliyoruhusu mabao machache zaidi hadi sasa katika Ligi Kuu ikifungwa mawili kama ilivyo kwa Azam na yote yakipatikana kwenye mchezo iliyopoteza ugenini mbele ya Ihefu SC, kuonyesha timu hiyo kwa msimu huu ina ukuta mgumu usiopitika kirahisi.

Kikosi hicho ni kati ya timu ambazo hazikubangua sana ukuta wake na hilo limekuwa nguzo ya kuifanya ianzie ilipoishia.

Ukuta wa Yanga una maingizo matatu pekee, Yao Kouassi na Nickson Kibabage ambao wamekuwa na uhakika wa kutumika mara kwa mara kulinganisha na mwenzao Gift Fred ambaye hajawa na uhakika hadi sasa.

Langoni Yanga bado inalindwa na Kipa Bora wa misimu miwili nfululizo iliyopita, Djigui Diarra lakini mbele yake kuna mabeki watatu wa kati wenye ubora Ibrahim Hamad ‘Bacca’, nahodha mkuu Bakar Mwamnyeto na msaidizi wake, Dickson Job.

Mabeki hao watatu wa kati Yanga inavuna faida kubwa kwa kuwa pia mabeki wanaoichezea timu ya taifa Tanzania wanaoitwa kwa pamoja katika kikosi cha Taifa Stars, huku mabeki wa pembeni wakiwa Joyce Lomalisa akisaidiana na Kibabage wakati kulia kuna mtu-kazi Yao Kouassi Attohoula ambaye alisajiliwa pia msimu huu.

Ujio wa Yao umeiongezea Yanga kitu kikubwa kutokana na ubora wa beki huyo mwepesi kukaba vizuri na kupandisha mashambulizi akiwa ameshafunga bao moja huku akitoa asisti tatu za mabao ndani ya mechi tano za ligi. Hapo ni mbali na Kibwana Shomary ambaye pia ni beki king’ang’anizi wa pembeni.

VIUNGO WA MABAO

Eneo jingine lililoibeba Yanga kwa kiasi kikubwa msimu huu ni pale katikati, kwanza wana nguzo mbili nzito zinazocheza mbele kidogo ya mabeki wawili wa kati Khalid Aucho na Mudathir Yahya ambao huifanya safu yao ya ulinzi kutofikiwa mara kwa mara.

Kwenye ubora wa viungo hao wawili bado wakaongezeka wenzao watatu wanaocheza mbele yao kama viungo washambuliaji Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli waliosajiliwa msimu huu na Stephanie Aziz KI.

Viungo hawa watatu ukiacha ubora wao wa kuifanya Yanga kuwa na kasi ya kushambulia kwa pasi zao za haraka, pia wamekuwa wakifunga na katika mechi tano za ligi wamefunga jumla ya mabao 9, kila mmoja akifunga matatu. Mudathir naye amefunga mawili hadi sasa katika mechi hizo tano za Ligi Kuu.

Ubora wao umekuwa ukiwafanya wapinzani kupata shida hasa wanapoanza kwa pamoja wakiwa pia na ubora wa kupiga pasi za mabao.

MZIZE, MUSONDA

Licha ya mshambuliaji Clement Mzize kutofunga bao lolote katika Ligi, lakini kasi yake imekuwa na tija ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na jinsi alivyoanza msimu akiwa ametangulia kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa akiwa na mabao matatu yakiwamo mawili aliyoifunga Al Merrikh ya Sudan nje ndani na kuivusha timu hiyo makundi ya CAF-CL tangu ilipofanya mara ya kwanza mwaka 1998.

Mbali na Mzize yumo Kennedy Musonda, ingawa amekuwa akikosa muendelezo mzuri akiwa ameshafunga bao moja kwenye ligi bado amekuwa na mchango wa kuipaisha Yanga hasa kupitia mfumo ambao wanautumia sasa chini ya kocha mpya Miguel Gamondi.

MBINU ZA GAMONDI

Kitu kingine kinachoibeba Yanga ni mbinu za Gamondi, kwani licha ya kocha huyo kuendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 lakini amekuja na kitu kipya ambacho ndio kinawaumiza wapinzani ambacho ni hatua ya timu hiyo kukaba zaidi tena wakianzia kule mbele kisha eneo la kiungo.

Yanga imekuwa na nidhamu ya kutaka mpira muda mwingi kuwa kwenye umiliki wake kuliko wapinzani wao ambapo endapo utakutana nao kwenye uwanja mzuri watakupa shida kama ambavyo imetokea kwenye mechi tano za ligi, licha ya moja ya ugenini dhidi ya Ihefu kulala 2-1.

Ndani ya nidhamu hiyo kuna kazi kubwa ya kocha wa viungo Taibi Lagrouni inaonekana ndani ya kikosi hicho ambapo timu hiyo imekuwa na ubora mkubwa wa kucheza kwa kiwango kilekile.

WASIKIE WADAU

Winga wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila alisema Yanga imekuwa na kasi katika kushambulia tofauti na msimu uliopita huku ubora mkubwa ukiwa ni eneo la katikati wanalocheza viungo.

Naye kiungo mshambuliaji Sekilojo Chambua amesifia usajili wa beki Yao kwamba umeongeza kitu kikubwa kwenye safu ya ulinzi kwa kuwa na mtu bora zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live