Beki Mtanzania, Emily Mugeta anayecheza soka nchini Ujerumani ametwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Nne (Verbandsliga) akiwa na timu yake ya Offenburger FV huku wakibaki na mechi moja mkononi dhidi ya FC Denzlingen itakayochezwa kesho Jumamosi.
Mugeta ambaye amecheza mechi 26 kati ya 31 ambazo timu yake imecheza hadi sasa ikibakiza moja kutimiza mechi 31 pia mkataba wake unamalizika Juni 30 mwaka huu tayari ameanza kufukuziwa na timu nyingine.
Offenburger FV imetwaa ubingwa huo ikiwa imekusanya pointi 65 ambazo haziwezi kufikiwa na mpinzani wao FC Denzlingen ambao pia ni miongoni mwa timu zinazofukuzia saini ya Mtanzania huyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Ujerumani, Mugeta alisema; “Tumebakiza mechi moja kumaliza ligi lakini tayari tumetwaa ubingwa kwa sababu pointi zetu ni nyingi kuliko timu nyingine hata wapinzani wetu wanaotufukizia hawawezi kutufikia na ni hao tunaomaliza nao mechi wao wana pointi 59.”
Kuhusu mkataba wake, alifafanua; “Tupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya, wanataka kunipa mkataba wa miaka miwili lakini bado tunabishana upande wa masilahi, kama wataboresha masilahi basi nitabaki na si vinginevyo.
“Kuna timu zinanihitaji ikiwemo hiyo tutakayocheza nayo mechi ya mwisho ya ligi, lakini kipaumbele ni hii timu yangu kwani kikubwa wanachotaka kukiboresha ni bonasi hata mshahara walipe miezi 11 maana mwezi wa 12 ligi huwa inasimama hivyo hawalipi kitu ambacho nimekikataa,” alisema.