Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtake msitake, mtapigika

Wanachama Pic Data Wanachama wa Simba

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hamtoki! Hiyo ni kauli ya wanachama wa Simba kuelekea mchezo wao na watani zao Yanga utakaochezwa Desemba 11, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na wanachama wa Simba, Wekundu wa Mtoni Mtongani kwa kile walichodai kuwa Yanga wajipange maana hawachomoki siku hiyo.

Katibu Msaidizi wa tawi hilo Uwesu Mafunga alisema kuwa timu hiyo haishikiki kwa sasa hivyo wapinzani wao wana kazi kubwa ya kufanya kuelekea mchezo huo.

“Tutakachowafanya Yanga hawataamini maana tunaenda kuwafunga na tunakaa juu ya msimamo baada ya hapo ndipo watajua kuwa ubingwa tuliochukua mara nne mfululizo hatujabahatisha,” alisema.

Mjumbe wa tawi hilo Amina Ally alisema kitu kikubwa kitakachowapa ushindi kwenye mchezo huo ni wao kuendelea kucheza tofauti na wapinzani wao Yanga.

“Wenzetu wao wametulia tu sisi tumecheza mechi za kimataifa hivyo miili ya wachezaji wetu bado ni ya moto, naamini kabisa hao hawatoki,” alisema.

Mjumbe mwingine wa tawi hilo, Masoud Nanguja alisema Simba sio timu ya kuchukuliwa kawaida hata kidogo kama wengi walivyoanza kusema hivyo zamu yao imefika.

“Tutakachokifanya ni kuonyesha ukubwa wetu tunatambua mechi hizi huwa hazitabiriki lakini kutokana na maandalizi yetu kuanzia wachezaji na benchi la ufundi tutawafunga,” alisema.

Naye Zaina Said alisema ushindi watakaoupata utawaziba mdomo wapinzani wao hivyo wanachokifanya ni kukimbiza mwizi kimya kimya.

“Hawataamini na macho yao tukiwafunga siku hiyo na kukaa kileleni hiyo ndiyo itakuwa ni safari yao ya mwisho kutupigia kelele mtaani,” alisema.

Tawi hilo lilianzishwa mwaka 2018, lina wanachama 250, likiongozwa na Mwenyekiti Shariff Abdallah, msaidizi wake Patrick Shelukindo, Katibu Mkuu Hugwa Mtumbatu, msaidizi Uwesu Mafunga, mtunza fedha Michael Tama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live