Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtajua wenyewe...

Mtajua Pic Data Mtajua wenyewe...

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Upepo haujakaa vizuri ndani ya Yanga kutokana na taarifa za kutaka kuondolewa kwa makocha Nasreddine Nabi na Cedrick Kaze lakini ushindi dhidi ya KMC leo Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku hapana shaka utarudisha nyuso za tabasamu kwa mashabiki wake.

Kwanza utawafanya wasogee kileleni mwa msimamo wa ligi wakifkisha jumla ya pointi 17 lakini kubwa zaidi ni kuwaweka kwenye presha kubwa watani wao Simba katika mchezo wa kesho dhidi ya Azam FC.

Ugumu wa mchezo wa kesho baina ya Simba wanaoongoza msimamo wa ligi na Azam FC walio nafasi ya sita, hapana shaka utaongeza ari ya na hamasa kwa Yanga kuhakikisha inapata ushindi leo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwaondoa watani wao kileleni mwa msimamo wa ligi ambako wametamba tangu katika raundi ya nne hadi sasa.

Hata hivyo, mabingwa hao watetezi watalazimika kuvuja jasho hasa ili wavune pointi tatu muhimu mbele ya KMC leo kutokana na kiwango bora ambacho wapinzani wao hao wamekuwa nacho katika siku za hivi karibuni tofauti na walivyoanza ligi.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Thiery Hitimana imekuwa ikicheza soka la kasi na pasi za harakaharaka kwenda langoni mwa timu pinzani pindi inapokuwa na mpira lakini inapopoteza, wachezaji wake wamekuwa na haraka ya kuziba mianya ili kutotoa nafasi kwa wapinzani kulisogelea lango lao haraka jambo ambalo limekuwa likiwasaidia kupunguza hatari za wapinzani.

Kwa upande wa Yanga, silaha yao kubwa ni safu yao ya kiungo ambayo pamoja na kucheza soka la taratibu la pasi nyingi, imekuwa ndio ikipika na kufunga idadi kubwa ya mabao ya timu hiyo katika ligi kuu hadi sasa.

Ushindi au sare ya mchezo wa leo licha ya kuifanya Yanga itinge kileleni mwa msimamo wa ligi, utaifanya pia izidi kuboresha rekodi yake ya kucheza mechi nyingi za Ligi Kuu bila kupoteza na itafikisha jumla ya michezo 44.

Ikiwa KMC wataibuka na ushindi, nao watasogea hadi kileleni mwa msimamo wa ligi kwani watafikisha jumla ya pointi 16 na kisha kuziombea nuksi Simba na Azam zitoke sare kesho ili yenyewe iendelee kushika nafasi hiyo.

Wakati Yanga wakiingia kwenye mechi ya leo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Simba, Jumapili iliyopita, KMC wenyewe wametoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, Ijumaa iliyopita.

Yanga imekuwa na historia nzuri dhidi ya KMC pindi zikutanapo na kudhihirisha hilo, imepata ushindi mara tano katika mechi nane walizowahi kukutana kwenye Ligi Kuu, wakitoka sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.

Kocha msaidizi wa KMC, Ahmad Ally alisema; “Kiujumla tuna maandalizi mazuri na vijana wako tayari kwa jinsi gani ambavyo tunakwenda kutumika. Tunajua kabisa tunakwenda kucheza mechi ngumu na timu bora. Sisi pamoja na wachezaji tunafahamu umuhimu wa mechi ya kesho (leo)”

Tunajua nini ambacho tunakwenda kukifanya. Hakuna mchezaji wetu mwenye shida na tuko tayari kwa mechi,” alisema Ally.

Kwa upande wa Nabi alisema; “KMC imezidi kuwa imara na bora msimu huu kutokana na kiwango ambacho imekuwa ikionyesha hasa kuanzia mechi dhidi ya Simba na Azam. Tumejiandaa vizuri na tunawaheshimu. Tumepata muda mchache wa kujiandaa baada ya mechi dhidi ya Simba lakini cha muhimu ni pointi tatu.” Mbali na mechi hiyo ya Yanga na KMC, mchezo mwingine wa Ligi leo utakuwa ni baina ya Ruvu Shooting itakayoikaribisha Geita Gold katika Uwanja wa Uhuru jijini kuanzia saa 10:00 jioni.

Chanzo: Mwanaspoti