Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtajua hamjui! Mgunda apiga mkwara, Minziro apania

BA125068 B593 4212 A3D3 EFAB6E6B9CE8.jpeg Mgunda na Clatous Chama

Sun, 18 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Simba na Geita Gold zinatarajiwa kushuka uwanjani jioni ya leo kwenye pambano la Ligi Kuu Bara, huku kila timu ikikabiliwa na mtihani wa kuhakikisha inaondoka na pointi tatu na makocha wake kutambiana.

Simba ya Juma Mgunda inakabiliwa na mitihani miwili kwenye mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa kuanzia saa 10:00 jioni.

Kibarua cha kwanza ni kusaka pointi tatu muhimu zitakazoiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi, ila cha pili ni kumaliza ubabe wa Geita kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Baada ya Azam kulazimishwa sare na Kagera Sugar, juzi kwenye Uwanja wa Kaitaba, ushindi wowote dhidi ya Geita utaifanya Simba ipande hadi nafasi ya pili na kuipumulia Yanga inayoongoza na usiku wa jana ilikuwa uwanjani kuumana na Polisi Tanzania.

Matokeo ya ushindi yataifanya Simba ifikishe pointi 37, moja zaidi ya ilizonazo Azam yenye pointi 36. Lakini kwa upande wa wenyeji Geita, ushindi utawafanya wafikishe pointi 25 na kurejea nafasi ya tano ikiipiku kwa tofautiywa mabao ya kufunga na kufungwa Mtibwa Sugar yenye idadi kama hiyo ya pointi.

Mtihani wa pili ambao Simba itapeta kama itaibuka na ushindi ni ule wa kuwa timu ya pili katika ligi kushinda dhidi ya Geita ugenini na kufuata nyayo za Yanga ambayo ndio pekee iliyoifunga wenye uwanja wa nyumbani.

Rekodi zinaonyesha tangu Geita ilipopanda daraja msimu uliopita, imepoteza mechi mbili za ligi nyumbani kati ya 23 ilizocheza ikiwa mwenyeji ambazo hizo zote mbili ni dhidi ya Yanga kila mchezo ilifungwa bao 1-0 na mechi 21 ni ama ilishinda au sare, pia imeshinda michezo 11 na kutoka sare 10, ikipachika mabao 30 na kuruhusu 17.

Simba imekuwa na historia nzuri dhidi ya Geita kwani katika mechi tatu walizokutana katika ligi imeshinda mara mbili na kutoka sare mchezo mmoja.

Mwendelezo wa kufanya vizuri katika mechi zao za hivi karibuni za ligi unaweza kuwa uthibitisho timu hizo zilivyo imara kwa sasa na kudhihirisha hilo, Simba imecheza mechi nane mfululizo za ligi bila kupoteza ikishinda sita na kutoka sare mbili, huku Geita ikiwa haijapoteza michezo mitano mfululizo ikishinda miwili na sare tatu.

Katika mchezo huo, Geita itawakosa Saido Ntibazonkiza anayetumikia adhabu ya kukosa mechi mbili na Raymond Masota na Edmund John ambao ni majeruhi kama ilivyo kwa Simba itakayowakosa Peter Banda na Israel Mwenda wanaojiuguza muda mrefu.

Simba itawategemea Moses Phiri mwenye mabao 10, Clatous Chama aliye kinara wa asisti akiwa na saba, sambamba na wakali wengine, ilihali Geita licha ya kumkosa Saido ambaye ndiye kinara wa mabao na asisti wa timu hiyo, bado ina wachezaji watakaoibeba akiwamo nahodha Danny Lyanga, Edmund John, Juma Liuzio na wengine.

MGUNDA, MINZIRO

Juma Mgunda, kocha wa Simba alisema: “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kushindana. Ni mechi ngumu, lakini tutahakikisha tunapambana ili kufanya vizuri, huku kocha wa Geita, Fred Felix ‘Minziro’ akisema watapambana ili kupata ushindi nyumbani.

Chanzo: Mwanaspoti