Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtaalamu aipa Yanga njia CAF

Khalil Ben Youssef Mtunisia Khalil Ben Youssef

Wed, 15 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga wajanja sana. Wakati wapinzani wake kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya Makundi, US Monastir ya Tunisia wakipiga hesabu za kutua Bongo wiki hii, tayari mtaalam wao amepata mbinu za kuhakikisha wanashinda mchezo huo utakaopigwa Jumapili ya Machi 19, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Monastir kimahesabu tayari imefuzu robo fainali, lakini Yanga inahitaji ushindi kwenye mechi dhidi ya Waarabu hao ili nayo ifuzu na kuzibwaga TP Mazembe ya DR Congo na Real Bamako ya Mali.

Mwanaspoti limeambiwa tangu wiki iliyopita benchi la ufundi kupitia kwa mtaalamu wa kuwasoma wapinzani aliyetua jangwani mwanzoni mwa mwezi huu, Mtunisia Khalil Ben Youssef ameshamaliza kazi yake na kugundua Yanga ilikosea wapi kupitia mikanda ya Monastir ikiwemo ule ambao Yanga ilifungwa 2-0 ugenini na michezo mingine ya timu hiyo.

Mtaalamu huyo ambaye aliwahi kufanya kazi hiyo akiwa na Esperance ya Tunisia, ameshachora ramani nzima ya mechi hiyo na kungundua kuwa Yanga wanatakiwa kufanya nini ili kushinda mechi hiyo.

Moja ya vitu ambavyo Yanga imebaini kutoka kwa Monastir ni kutokuwepo kwa kipa namba moja wa kikosi hicho Ben Said ambaye ana kadi tatu za njano na moja ya mawinga hatari wa kikosi hicho (ambaye hakutajwa jina) aliyepata majeraha mazoezini na ataukosa mchezo wa hapa Dar es Salaam, Jumapili ijayo.

Pia Yanga imebaini Monastir huenda kwenye kikosi cha kwanza watakachopanga dhidi ya Yanga Jumapili wakaanza na mabadiliko ya wachezaji watatu hadi wanne ilikutunza nguvu kwa ajili ya robo fainali kwani tayari wamefuzu, lakini pia wana vita kwenye ligi yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Youssef alisema wamebaini mambo mengi ndani ya Monastir lakini mengine yatabaki kuwa siri yao na wanaendelea kuyafanyia kazi kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kufuzu.

"Itakuwa mechi ngumu kwetu lakini tayari tumejua baadhi ya mipango ya wapinzani wetu hivyo tunaweza kuanzia hapo kuhakikisha tunashinda. "Siwezi kuweka kila kitu hadharani lakini jua tunachohitaji ni ushindi tu na tuna uhakika na hilo kutokana na mechi ilivyo na vitu ambavyo tunavyo hadi sasa," alisema Youssef ambaye anaamini kwa walivyojipanga, Yanga inatinga robo fainali.

Kocha Nabi pia alisema kimbinu Yanga inaendelea vizuri na kila mchezaji sasa anaelekezwa majukumu yake katika mechi hiyo ambayo anaamini wakiyatimiza kwa ufasaha, Monastir atafungika kwa Mkapa.

Nabi alisema katika mechi ya kwanza walifanya makosa wachache yaliyoigharimu timu kufungwa 2-0 lakini tayari wameyafanyia kazi na sasa wanaanda timu itakayowafanya Monastir wafanye makosa na kushinda.

"Hatuwaogopi licha ya kwamba ni timu nzuri, walitufunga kwao na sisi tuna uwezo wa kuwafunga hapa Tanzania, tunaendelea kujipanga ili tushinde na naamini tutafanya hivyo kama kila kitu kitaenda tulivyopanga," alisema Nabi anayesifika kwa mbinu nyingi kabla na wakati mechi ikiendelea.

Hadi sasa kundi hilo D, linaongozwa na Monastir yenye alama 10, ikifuatia Yanga yenye saba, TP Mazembe ni ya nne na pointi tatu huku Real Bamako ikishika mkia na pointi mbili na timu zote zimecheza mechi nne.

Chanzo: Mwanaspoti