Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva awakosha Morocco, anatupia tu

Msuva Pic Simon Msuva akifanya vitu vyake nchini Morocco

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa sasa Simon Msuva yupo Bongo, anajiandaa kukipiga na DR Congo kwa Mkapa Novemba 11.

Baada ya kufikisha jumla ya mabao 39 kwenye Ligi ya Morocco ambayo ni maarufu kama Batola Pro ndani ya michezo 84, wadau na mashabiki mbalimbali wa soka nchini humo, wamempigia saluti mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva kwa kusema ni mtambo wa mabao.

Mashabiki hao walishindwa kujizuia mara baada ya nyota huyo wa Tanzania kutupia mabao mawili wakati chama lake, Wydad Casablanca likiibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Olympique Khouribga, Jumatano ya wiki iliyopita kabla ya mchezo dhidi ya Raja Casablanca, Jumamosi.

Wakiongea na gazeti hili kwa njia ya mtandao, mashabiki hao kutoka Morocco, walionyesha kuvutiwa na kiwango cha mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga kwa kusema Msuva anaweza kwa kusaidiana na wachezaji wenzake kuifanya Wydad Casablanca kutwaa ubingwa wa Afrika.

Elmahdi Lfasi alisema mwanzoni hakuwa akimwelewa Msuva kwani alidhani pengine anaweza kuwa kama nyota wengine ambao walisajiliwa kutoka timu ndogo na kushindwa kufanya vizuri wakiwa na timu kubwa kitu ambacho kinaonekana kuwa tofauti kwa Mtanzania huyo.

“Kwa sasa sina shaka na uwezo wa Msuva maana tayari ameonyesha kuwa yeye ni aina gani ya mchezaji, tangu msimu uliopita alikuwa akifanya vizuri, kasi yake imekuwa ikitusaidia kule mbele na kwa bahati nzuri ni mmaliziaji mzuri,” alisema mdau huyo.

Kwa upande wake, Hamza Mateech alisema amekuwa akimfahamu Msuva tangu akiwa Difaa El Jadida maana mara kadhaa aliwahi kuifunga Wydad Casablanca hivyo hilo lilitosha kwake kuona kuwa mshambuliaji huyo anaweza kuwa msaada kwenye klabu hiyo.

“Kiu ya mashabiki wa Wydad ni kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na ndio maana baada ya kocha wa msimu uliopita kushindwa kufikia malengo alifukuzwa maana hapa kuna karibu kila kitu, kikosi chetu kimekamilika, kina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa akiwemo Msuva,” alisema.

Mabao mawili ambayo Msuva alitupia Jumatano ya wiki iliyopita yalimfanya kuhusika katika mabao nane katika mechi 11 akifunga matano na kutoa asisti tatu tangu ajiunge na Wydad Casablanca msimu huu wa 2021/22 kwenye mashindano yote, ikiwemo Ligi ya Mabingwa.

Wikiendi iliyopita, Msuva alicheza mchezo wake wa kwanza wa dabi msimu huu ambao ni dhidi ya Raja Casablanca uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kurejea zake Tanzania kwa majukumu ya timu ya taifa ambayo Alhamisi ina mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia.

Msuva alirejea jana, Jumapili na huenda akaungana na wachezaji wenzake wa Taifa Stars leo au kesho kwa ajili ya maandalizi ya kuwavaa DR Congo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live