Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva ataka ufalme Iraq

Msuva Mnsz Simon Msuva

Sun, 8 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva (30), ameeleza mikakati yake wakati akianza safari mapema leo, Ijumaa kwenda Iraq kwa ajili ya kujiunga na chama jipya la  Al Talaba SC.

Msuva ambaye alikuwa nchini kwa zaidi ya miezi mitatu tangu kumalizika kwa msimu uliopita ambao alikuwa akiichezea Al-Najma  ya Saudi Arabia, alisema hii ni fursa nyingine tena kwake kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi.

“Nina uzoefu wa kutosha kwa hiyo nahitaji kuendeleza kile ambacho nimekuwa nikikifanya kwa miaka mingi. Al Talaba walinitafuta baada ya mkataba wangu kumalizika kule Saudia na nikawaeleza mahitaji yangu na kwa bahati nzuri walikuwa tayari kunipa nilichohitaji,” alisema mchezaji huyo.

“Kilichobaki kwa sasa ni mimi tu kuwafanyia kazi yao. Binafsi sina shaka na uwezo wangu nipo tayari kuonyesha Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye vipaji vingi  vya soka. Nina shauku kubwa ya kuanza maisha yangu mapya ya utafutaji Irak najua ni nchi nzuri kama ilivyo Saudia.”

Kulingana na programu za mazoezi ambazo alikuwa akitumiwa, Msuva anaamini zitamsaidia kuwa katika mstari mmoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.

“Mbali na ratiba ya timu nilikuwa nikijisukuma mwenyewe kila siku ili niwe bora zaidi na hilo limekuwa likinisaidia. Binafsi nimejiandaa kutumika katika nafasi yoyote ambayo benchi la ufundi litapenda kunitumia.”

Al Talaba itakuwa timu ya sita kwa Msuva kuichezea nje ya Tanzania, chama lake la kwanza lilikuwa Difaa El Jadida alilojiunga nalo Julai 2017 baada ya kuonyesha makali yake ndani ya miaka mitatu kwenye Ligi ya Morocco, Wydad Casablanca ilijivunia naye na kumsajili lakini hakudumu kwa vigogo hao kutokana na ishu za madai zilizowafanya kufikishana Fifa.

Baadaye Msuva aliibukia Saudi Arabia ambako alianza kwa kuichezea Al-Qadsiah mkataba wake ulipomalizika alirejea Afrika kujiunga na JS Kabylie ya Algeria, lakini mambo hayakumwendea vizuri mkataba wake ulikatishwa na ndipo alipoamua kurejea tena Saudia Arabia ambako alijiunga na Al-Najma aliyoichezea  katika msimu uliopita wa mashindano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live