Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva apewe maua yake Stars

Msuva.jpeg Msuva apewe maua yake Stars

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Saimon Msuva inawezekana akawa ni mchezaji ambaye hana kipaji kikubwa sana cha soka, lakini kucheza kwake kwa kujitolea ni silaha ambayo imekuwa ikimbeba.

Na kwa bahati nzuri, Msuva amekuwa akijitolea pindi anapokuwa akicheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambapo amekuwa akiifungia mabao muhimu kwenye mechi za mashindano tofauti ambayo imekuwa ikishiriki.

Kwa mfano katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon mwaka huu, Taifa Stars ilipachika mabao matatu tu katika mechi sita na katika mabao hayo, Saimon Msuva alifunga mawili hivyo kwa maana yake bila yeye Tanzania isingefuzu kwenda Ivory Coast.

Katika fainali hizo za Afcon mwaka huu, Taifa Stats ilifunga bao moja tu katika mechi tatu na lenyewe liliwekwa kimiani na Msuva ambaye hadi anakwenda Ivory Coast alikuwa mchezaji huru.

Ikumbukwe kwamba Msuva ndiye mchezaji pekee wa Tanzania kufunga bao katika awamu mbili tofauti za Afcon ambapo alifanya hivyo mwaka 2019 zilipofanyika Misri na pia akaja kutungua tena kipa katika fainali za mwaka huu.

Msuva anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wetu wa Kitanzania kwa kuhakikisha wanacheza kwa kujitoa na kupigania vilivyo jezi ya Taifa Stars ili waweze kuweka alama kama ambavyo nyota huyo wa zamani wa Yanga amekuwa akifanya.

Wapo baadhi ya wachezaji ambao wanapokuwa wanaichezea Taifa Stars wanaonekana wazi hawana ile ari ya kuipambania kama ambavyo wamekuwa wakifanya hivyo katika klabu zao.

Wanachosahau ni kwamba timu ya taifa ni mahali pazuri pa kumbeba mchezaji kwa maana ya wasifu wake kwani klabu nyingi za nje hutoa kipaumbele cha kusajili mchezaji ambaye anaitumikia timu yake ya taifa.

Msuva huyohuyo anaweza kuwa mfano kwani kabla hata fainali za Afcon hazijamalizika na Taifa Stars kutolewa, amesajiliwa na Al Najmah inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia.

Chanzo: Mwanaspoti