Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva alivyobadili gia Yanga

Smsuva27 1692777281380.jpeg Simon Msuva

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wananchi walikuwa wakifurahia taarifa za mshambuliaji wao wa zamani, Simon Msuva kuwa kwenye nafasi kubwa ya kurejea nyumbani ‘Jangwani’ baada ya kuachana na JS Kabylie ya Algeria

Pamoja na vuta nikuvute ya mazungumzo kati ya mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Tanzania na viongozi wa timu hiyo hawakufikia mwafaka hadi dirisha la usajili nchini lilipofungwa.

Hata hivyo, kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, Januari 15 haikuwa ishu kwa Msuva na hata upande wa viongozi wa Yanga kwani waliamini wanaweza kumsajili mchezaji huyo kupitia mlango wa kwamba ni mchezaji huru pia ni mzawa na hata hivyo alikuwa kwenye majukumu ya kitaifa, Shirikisho la soka nchini (TFF) na Bodi ya ligi ingetoa baraka zote kwenye hilo.

Viongozi wa Yanga waliongea na Msuva mara tu baada ya kupata taarifa mchezaji huyo kwa wakati huo anapatikana, kwa mujibu wa taarifa inaelezwa supastaa huyo aliwaambia wasubiri ili afanye majadiliano na familia yake.

Pamoja na kupewa ofa nono na Yanga, Msuva alikuwa na hesabu zake kichwani hivyo kuchelewa kwake kutoa majibu ya moja kwa moja kuliwafanya viongozi wa timu hiyo kuendelea na mipango yao mingine ya usajili ikiwemo kuleta mshambuliaji mpya wa kati, Joseph Guede kulingana na mahitaji ya timu.

Hesabu ambazo Msuva alikuwa nazo kichwani ni kuonyesha kiwango kizuri kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ili kupata ulaji kitu ambacho alifanikiwa japo Taifa Stars iliishia kwenye hatua ya makundi huko Ivory Coast.

Huyu hapa Msuva anaeleza,”Kiukweli kabisa najiona nina uwezo wa kuendelea kucheza soka la ushindani nje ya nchi, natamani kupambana na hata baada ya kukumbana na changamoto Algeria sikuona kama ndio umefika mwisho, kila kocha anayekuja kwenye timu huwa na mipango yake, unaweza kushindwa kuendana na huyu kwa yule ukawa mchezaji muhimu ni mambo ya kawaida kwenye mpira.”

Anaendelea Msuva kwa kusema wakati anaenda Afcon alijua hilo ni jukwaa ambalo linaweza kumfanya kupata timu nyingine maana hayo ni mashindano makubwa ambayo yamekuwa yakifuatiliwa na mawakala kutoka sehemu mbalimbali.

“Nashukuru Mungu sana kwa sababu kile ambacho tulikuwa tukikipigia hesabu na watu wangu kimetimia, narudi tena Saudia kuendelea na mapambano, pamoja na ugumu wa mashindano nilijitahidi sana kujitoa ili kulisaidia taifa langu, pia kuonyesha uwezo wangu kama mchezaji,” anasema.

Msuva ndiye mchezaji pekee wa Tanzania aliyefunga bao kwenye fainali hizo, alifanya hivyo kwenye mchezo ambao Taifa Stars ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia, ilikuwa mechi ya pili kwenye mashindano baada ya kwanza kufungwa dhidi ya Morocco kwa mabao 3-0.

Bao alilofunga ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kufunga bao kwenye fainali mbili tofauti za Afcon, ikumbukwe katika mashindano yaliyofanyika Misri alifunga bao kwenye mchezo dhidi ya Kenya ambao tulipoteza kwa mabao 3-2 kwenye wanja wa June 30, Cairo.

Al-Najma Sport Club ambayo amejiunga nayo Msuva ni timu ya soka huko Saudi Arabia yenye makao yake makuu Unaizah, chama hilo lipo Ligi Daraja la Kwanza la Saudia. Ilianzishwa mwaka 1960, imekuwa ikitumia rangi nyeupe, nyeusi na rangi ya kijani kwenye jezi zao za nyumbani na ugenini.

“Hii sio timu ngeni kwangu kwa sababu wakati nikiwa Saudia nilicheza ligi daraja la kwanza, naamini wananifahamu kwa sababu nilifanya vizuri wakati nikiwa nchini humo kipindi nilichokuwa nacheza kwa mara ya kwanza,” anasema.

Al-Najma aliyojiunga nayo Msuva mahasimu wao huko Saudia ni Al-Arabi, timu hizo zikikutana huwa ni mechi ngumu na ya kuvutia kutokana na upinzani mkali uliopo kati yao na mchezo baina yao huitwa Unaizah Derby.

Wakati Msuva akiwa Saudia kwa mara yake ya kwanza kucheza soka la kulipwa nchini humo, alikuwa akiitumikia Al-Qadsiah ambayo inapatikana katika mji wa mashariki wa Khobar na uwanja wao wa nyumbani ulikuwa Prince Saud bin Jalawi.

Al-Najma itakuwa timu ya tano kwa Msuva kuichezea nje ya mipaka ya Tanzania, alianza safari yake hiyo kwa kuichezea Difaa El Jadida ya Morocco baada ya kuuzwa na Yanga 2017, kufanya kwake vizuri akiwa na timu hiyo ndogo kuiifanya miamba ya soka nchini humo, Wydad Casablanca kuvutiwa naye.

Msuva alikuwa na maisha mazuri akiwa na Wydad Casablanca lakini changamoto za nje ya uwanja zilimtibulia na kuingia kwenye mvutano na wababe hao hadi kupelekana FIFA ambako mshambuliaji huyo wa Kitanzania alitakiwa kulipwa stahiki zake na huo ndio ukawa mwisho wake na timu hiyo ambayo ndani ya msimu huo ilitwaa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ndipo Msuva alipoamua kwenda zake Saudia kwa mara ya kwanza kabla ya kurejea zake Afrika kwa kujiunga na JS Kabylie ya Algeria.

“Nimejifunza vitu vingi sana kwenye maisha ya soka nje ya nchi, mengi nimevulimia kwa sababu huu ni mchezo ambao naupenda, bado nitaendelea na mapambano na wakati ukifika wa kurudi nyumbani, nitarudi na kumalizia soka langu,” anasema Msuva.

Kurejea kwa Msuva huko Saudia, kumebeba matumani ya mashabiki wa Al-Najma ambao chama lao lipo katikati mwa msimamo wa ligi hiyo.

Ligi Daraja la Kwanza Saudia imeingia kwenye raundi ya pili hivyo timu zimeanza kujipambanua ili kupanda ligi kuu ambako kunamastaa kibao wakubwa kwenye soka duniani kama vile Cristiano Ronaldo anayeichezea Al Nassr.

Chanzo: Mwanaspoti