Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva aewaita Yanga mezani

Msuva JS Kabylie Simon Msuva.

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Winga wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Simon Msuva, amethibitisha kuwa amemaliza mkataba wake na Klabu ya Al Najma ya Saudi Arabia, hivyo kuzifungulia mlango Klabu za Yanga, Simba na Azam FC kumsajili kama zinahitaji huduma yake.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Msuva alisema mkataba wake na klabu hiyo ulikuwa ni wa msimu mmoja tu, hivyo sasa yupo huru kujiunga na klabu yoyote inayomhitaji, lakini aliwaambia mashabiki wake kutulia kwani chochote kitakachotokea atawaambia.

"Mkataba kule nimemaliza chochote kitakachotokea nitawajulisha, sitaki kuongelea habari zozote kuhusu ofa kwa sasa, zipo nyingi ila muda ukifika nitawajulisha, kikubwa mashabiki wangu waelewe bado nipo Saudi Arabia, kuna timu nyingi kule za kuchezea, lakini pia kuna ofa kutoka sehemu mbalimbali Afrika, hivyo chochote kitakachotokea kipya basi Watanzania watakiona kwa upande wangu," alisema mchezaji huyo ambaye kabla ya timu hiyo alikuwa akiichezea JS Kablie ya Algeria.

Hivi karibuni Klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikihusishwa kutaka kumsajili mchezaji huyo hasa kipindi hiki cha dirisha la usajili, ambaye mara ya mwisho kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni msimu wa 2017, akiwa na Klabu ya 'Wananchi.'

Msuva ambaye ni mmoja wa wachezaji wakongwe na tegemeo kwenye kikosi cha Stars, alianza karia yake ya soka katika kikosi cha Azam FC, 2010 hadi 2011, kabla ya kutimkia Moro United ambapo alicheza msimu mmoja, 2011 hadi 2012 na kutua Yanga, alipoichezea hadi 2017.

Mchezaji huyo alianza safari yake ya soka la kulipwa 2017 alipojiunga na Diffa el Jadida ya Morocco, hadi 2020 alipotimkia Wydad Casablanca ya huko, 2022 hadi 2023 akaichezea Klabu ya Al Qadsiah ya Saudia Arabia, baadaye JS Kablie na Al Najma.

Hata hivyo, wakati dirisha la usajili likiwa limefunguliwa usiku wa kumkia Jumamosi, Klabu za Yanga, Singida Fountain Gate, Tabora United, Biashara United na FGA Talents zimezuia kusajili mpaka pale zitakapowalipa wachezaji wanaozidai.

Taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), ikisainiwa wa Ofisa Habari na Mawasiliano wake, Cliford Ndimbo, imesema kuwa klabu hizo zimefungiwa kwa pamoja na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na TFF, hivyo haziwezi kuingiza mchezaji yoyote kwenye mfumo wa usajili wa kimataifa

"Klabu ambayo itawalipa wahusika, itaondolewa mara moja adhabu ya kufungiwa kusajili," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

TFF imesema mpaka jana asubuhi, hakuna klabu yoyote kati ya hizo iliyowalipa wahusika, ikiwakumbusha kufanya hivyo, vinginevyo hawatoweza kufanya usajili.

Yanga hivi karibuni, FIFA na TFF iliifungia kwa kutomlipa aliyekuwa mchezaji wake, Hafiz Konkoni raia wa Ghana ambaye alipewa mkono wa kwaheri katikati ya usajili wa msimu uliopita, baada ya kusajiliwa mwanzoni mwa msimu huo.

Hata hivyo, Yanga imewatoa hofu wanachama na mashabiki kuwa itatekeleza maagizo hayo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema klabu hiyo italipa madeni ya wachezaji wote wanaodai, hata wale ambao itawapa mkono wa kwaheri msimu huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live