Nyota wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amesema Ligi ya Saudi Arabia ni ngumu tofauti na watu wanavyodhani kwani Waarabu wamewekeza na mchezaji yoyote mkubwa wakimtaka wanamchukua hivyo ushindani ni mkubwa.
"Timu niliyokuwa nacheza [Saudi Arabia] inashiriki Ligi ya Champioship sio Ligi Kuu, ikitoka Ligi Kuu wanayocheza kina Ronaldo Ligi inayofuata ndio nilikuwa nacheza mimi pamoja na timu ya Pitso Mosemane ambayo alifanikiwa kuipandisha Ligi Kuu.
"Ligi ya juu ni ngumu lakini hata Ligi niliyokuwa nacheza [Championship] ni ngumu vilevile, wanasema Ligi ya Saudi Arabia ni ngumu ukilinganisha na Qatar. Hata mimi kabla sijaenda nilikuwa nahisi watu wanaenda kuvuna pesa lakini pesa yao unaifanyia kazi.
"Niwaweke watu wazi kuhusu Ligi na soka la Saudi Arabia, kule watu hawaendi kumalizia soka kama ambavyo wengi wanafikiri, watu wanacheza kweli.
"Wenzetu wanajua nini maana ya biashara kwenye wa mpira wa miguu, wamewekeza sana wakihitaji mchezaji yeyote wanamchukua," amesema Msuva.