Mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva amesema mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023 yamemsaidia kupata timu mpya baada ya kuachana na timu aliyokuwa akiitumikia kabla ya mashindano hayo.
“Nimetoka kwenye matatizo na ile timu yangu ya JS Kabylie ya Algeria lakini nilijua mimi kabisa siwezi kukosa timu na ndiyo maana nikasema huku ninakokwenda [AFCON] ndiyo nitajiuza, nitajitangaza ili niweze kupata timu,” amesema Msuva.
Msuva amesema alikuwa na ofa kutoka vilabu mbalimbali ikiwemo kutoka Uturuki, China na Iraq lakini ameichagua Al Najma inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Saudi Arabia kwa sababu anaifahamu ligi hiyo.
Kuhusu AFCON amesema ilikuwa ni matamanio yao kufuzu hatua ya 16 bora, lakini hawakufanikiwa, hivyo kilichobaki ni kujipanga zaidi kwa mashindano yajayo ili wafanye vizuri.
Tanzania imetolewa ikiwa na alama mbili ambapo ilipoteza mchezo dhidi ya Morocco, ikatoka sare na Zambia na kutoka suluhu na DR Congo.