Wakati mashabiki na wanachama wa Yanga wakiwa na hofu juu ya hatma ya mshambuliaji wao hatari raia wa Congo DR, Fisto Mayele, kama ataendelea kuwepo msimu ujao, mwanchama wa klabu hiyo na Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku 'Musukuma' amedokeza alichozungumza na Rais wa Klabu hiyo, Hersi Said juu ya hatma ya mkongomani huyo.
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Wiki ya Mwananchi, Musukuma amesema kuwa amekuwa akifanya mazungumzo ya mara kwa mara na Rais Hersi ambaye amemuhakikishia kuwa wananchi wataendelea kupata burudani ya kutetema msimu ujao.
Bila kutaja jina la Mayele, Musukuma ametumia lugha ya ishara akionyesha stairi ya ushangiliaji ya Mayele huku mashabiki na wanachama wa timu hiyo waliojitokeza katika uzinduzi huo uliofanyika Furahisha Wilayani llemela mkoani Mwanza, wakimuunga mkono kwa kutetema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Yanga, Yanga Makaga naye amekazia kauli ya Musukuma kwa kusema kuwa msimu ujao mashabiki na wanachama wa timu hiyo wataendelea kutetema.