Klabu ya Simba, imeingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Pablo Franco raia wa Hispania mwenye miaka 41, akichukua mikoba ya Mfaransa, Didier Gomes aliyesitishiwa mkataba wake hivi karibuni.
Kabla ya Pablo kujiunga na Simba, alikuwa akiinoa Al Qadsia SC ya Kuwait kuanzia 2019 hadi 2021.
Rekodi zinaonesha kwamba, mwaka 2015, Pablo alikuwa Kocha Mkuu wa Getafe inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania maarufu La Liga.
Pablo ambaye ni muumini wa soka la kushambulia kama nyuki pindi anapoamua kutafuta ushindi, alikuwa kocha msaidizi wa Real Madrid mwaka 2018 chini ya Julen Lopetegui na baadaye Santiago Solari.
Pamoja na kuwa muumini wa soka la kushambulia, Pablo anamudu umiliki wa mpira kwa staili ya Hispania ya pasi nyingi maarufu tik taka, staili ambayo anapoileta Simba, tutashuhudia soka safi Uwanja wa Mkapa, Dar, sehemu ambayo inaruhusu mchezaji yeyote kucheza anavyotaka kulinganisha na viwanja vingine nje ya Dar.
Kocha huyo ni msoni haswa kwani ana elimu ya Uefa pro na elimu ya juu ya viungo na usomaji wa michezo.
Kwa namna takwimu zake zilivyo, ni wazi kama nyota wa Simba wataingia haraka kwenye mfumo wake, basi vilio vya mashabiki wa timu hiyo vitakwisha na furaha itarudi upya kama ilivyokuwa msimu uliopita na mingine nyuma ambapo walitawala kwa kubeba mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara.
Msimu huu, Simba haikuanza vizuri ambapo katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, imeshinda tatu huku ushindi wenyewe ukiwa ni wa kubahatisha. Sare zikiwa mbili, hawajapoteza.
Katika mechi hizo tatu walizoshinda, Simba imefunga mabao matatu pekee kitu ambacho si kawaida yao kutokana na msimu uliopita walimaliza vinara wa mabao kwa kufunga 78 baada ya mechi 34.
Muda mfupi baada ya kocha huyo kutambulishwa juzi, Wanasimba walionekana kuwa na matumaini makubwa naye wakiamini kwamba atakuja kuibadilisha timu yao na kucheza soka la kuvutia.
Kocha huyo mtihani wake wa kwanza ndani ya Simba, utakuwa ni dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Novemba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.