Kipa wa Yanga, Abuutwalib Mshery hatakuwa sehemu ya kikosi hadi msimu ujao kutokana na upasuaji wa goti aliofanyiwa huko Tunisia.
Juzi, Mshery alirejea sambamba na timu yake ambayo ilikwenda nchini humo kucheza mchezo wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Terminal 3, kipa huyo alisema hali yake kwa sasa ni nzuri lakini atakuwa nje kwa kati ya miezi minne hadi mitano.
“Nitakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitano baada ya huu upasuaji. Awali nilishakaa nje kwa miezi miwili na nusu,” alisema.
Mshery aliongeza akisema; “Mpira huu dah. Nitaumisi kimtindo.”
Kipa huyo alikuwa anatembea kwa magongo mawili akiongozana na daktari wa timu hiyo, Youssef Ammar.
Timu hiyo baada ya Mshery kuumia ililazimika kumchukua kwa mkopo Metacha Mnata kutoka Singida Utd hadi mwishoni mwa msimu.