Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshery, Diarra mbona kazi ipo

Makipa Walinda wa Yanga

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanajiandaa kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa raundi ya nne ya michuano ya ASFC, lakini kocha wa makipa wa timu hiyo, Mbrazili, Milton Nienov akifichua vita nzito kati ya makipa wake.

Yanga kwa sasa ina makipa wanne, Diarra Djigui aliyepo na Mali kwenye fainali za Afcon 2021, Abuutwalib Mshery, Erick Johola na kipa chipukizi, Yunus Magaigwa na kumfanya kocha Nienov kukuna kichwa juu ya kipa chaguo la kwanza.

Kwa sasa Diarra ndiye aliyekuwa kipa namba moja, huku Johola akianzia benchi, lakini kwenda kwake Afcon kumemfanya Mshery aliyesajiliwa dirisha dogo kuanzishwa, huku Johola akiendelea kusubiri wakati mwingine na Magaigwa.

Hata hivyo, Nienov aliyetua Jangwani hivi karibuni wiki kadhaa tangu alipotemwa na Simba, alisema amepata nafasi ya kuangalia video za Diarra katika mechi mbalimbali alizocheza na anastahili kuwa chaguo la kwanza.

Milton alisema, Diarra ni kipa mwenye uzoefu mzuri katika kudaka na si wale wanatema mipira, anaweza kucheza mguuni jambo ambalo makipa wengi wanalikosa na shida alizonazo ni chache.

Alisema, Diarra atakaporejea kwanza ataboresha zaidi vilivyo bora kwa upande wake na baada ya hapo atamuelekeza na kumpa mbinu mbalimbali za kutibu udhaifu wake.

“Kuhusu Mshery nimewahi kufundisha makipa vijana katika maeneo mbalimbali ila huyo ni mmoja kati ya wale bora niliokutana nao, ana sifa nyingi za kipa bora halafu bado umri wake ni mdogo,” alisema Milton na kuongeza;

“Nikiangalia makipa wazawa huyo, Mshery anaweza kuja kumpa ushindani wa kutosha, Aishi Manula katika siku za usoni kutokana na vitu alivyonavyo kwenye kutimiza majukumu yake.”

Kocha huyo alisisitiza; “Kutokana na umri wake Mshery kuna aina mbalimbali ya mazoezi ambayo nitaendelea kumpatia, akiyashika na kufanya kwa nidhamu hata akiwa nje ya soka atakuja kuwa kipa bora kabisa katika taifa hili.

“Mshery anazo sifa zote zile za Diarra ila alichokosa ni uzoefu na kucheza mechi za presha kama mwenzake, akipata za aina hiyo mfululizo na akawa mzoefu atakuwa amekamilika zaidi,” Nienov alisema huku akisema anasubiri Diarra arudi ili kuona itakuwaje kwani hata akiwa nje bado lango lao lipo salama.

“Hata kama ikitokea siku Diarra hayupo Mshery atacheza tena bila shaka yoyote, kazi iliyopo kwao kwa sasa ni kufanyia kazi na kushika kwa ufasaha kila ambalo nawapatia mazoezini ili kuonyesha ubora zaidi kwenye mechi,” alisema Milton.

Mbrazili huyo aliwahi kufanya kazi kwa mahasimu wa Yanga, Simba kabla ya kutua Jangwani.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz