Kwa kipaji alichonacho kipa namba mbili wa Yanga, Aboutwalib Mshery ametakiwa akili yake ijikite kufanya ushindani wa kuonyesha kazi bora na siyo kujichukulia ziada anapokosekana Djigui Diarra.
Kipa wa zamani wa timu hiyo, Benjamin Haule alimwambia Mshery ana kipaji na kila nafasi anayopewa aichukulie kama ya kumpandisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine, anaamini akifanya hivyo thamani yake itakuwa kubwa.
"Jambo la msingi ajifunze kwa Diarra ana vitu gani vya ziada ili akipewa nafasi kocha awe anamwamini kwamba atamfanyia kazi yake bila presha, hakuna aliyezaliwa kipa namba moja ama mbili ni bidii yake mwenyewe.
"Ukiachana na huyo, Simba kuna Beno Kakolanya naamini akipata mechi nyingi anaweza akawa kipa namba moja, kikubwa wasione kukaa benchi hawana majukumu, badala yake wawe tayari ili wakipata nafasi wafanye makubwa zaidi."
Kocha wa timu za vijana za Yanga, Fredy Mbuna anawaibia siri wachezaji wote wanaoanza benchi kwamba wao ni suluhisho la kutibu udhaifu pindi timu inapokosa matokeo ya ushindi.
"Iwe kwa straika kama timu inahitaji ushindi basi anaangalia aliyeanza kafeli wapi, beki vilevile timu inaweza ikawa inaongoza inahitaji kulinda ushindi ama inashambuliwa sana basi kazi yake ni kuzuia kwa kipa vilevile, kikubwa wanaokaa benchi ili mladi wapo kwenye timu wasijione dhaifu badala yake wajue wana kazi kubwa," alisema.