Siku chache baada ya kuripotiwa kuwa kiungo Jonas Mkude anakaribia kumalizana na matajiri wa Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja, imebainika kuwa dau alilopewa staa huyo, lakini wakimbana kwelikweli kwa mambo manne.
Mkude anatajwa kukaribia kumalizana na Yanga zikiwa ni siku chache tangu alipoachana na Simba baada ya mkataba wake kumalizika, akiwa amedumu kwenye timu hiyo kwa miaka 13.
Mkude amewekewa dau la million 60 kwa miaka miwili lakini kwa kipengele cha kusainiwa mwaka mmoja kwa kwa dau la milioni 30 na kuongezewa mwaka mmoja endapo ataonyesha kiwango kizuri.
Mbali na dau hilo la usajili kiungo huyo pia ameahidiwa kitita cha shilingi milioni 10 kwa mwezi ambao ndiyo utakuwa mshahara wake wa kuitumikia timu hiyo, ikiwa na maana kwa miezi 12 atazoa milioni 120 Jangwani.
Mkude ambaye ameitumikia Simba kwa mafanikio akitwaa mataji 16 ndani ya misimu 13 aliyocheza pamoja na ahadi nzuri alizopewa amewekewa masharti makali ili kuweza kuendana na falsafa ya klabu hiyo.
"Ni kweli Mkude amepewa dau hilo la milioni 60 lakini atapewa 30 kwa ajili ya msimu mmoja ambao una kipengele cha kuongezewa mwingine endapo atafanya vizuri na kutimiza masharti ya mkataba kilisema chanzo.
"Mshahara wake ni milioni 10 kwa mwezi ofa hizo zimeambatana na masharti zaidi ya matatu ikiwa ni pamoja na nidhamu nje na ndani ya uwanja.
"Kila kitu wameshakubaliana, kilichobaki ni kuweka saini tu na hata watu ambao Mkude alitaka kuwapa mkataba wasome wameshasoma na kukubali.
"lakini Yanga wamekuwa wajanja, kuna vipengele nafikiri ni vinne wamembana kuhakikisha hawavurugi na vyote vinahusika na faini kama akivifanya.
"Jambo la kwanza ni kipengele cha nidhamu, anatakiwa kutofanya jambo lolote la utovu wa nidhamu akiwa kambini, nje ya kambi, kwenye mechi au mazoezini.
"Ameelezwa kuwa akifanya hivyo, atakatwa fedha kwenye mshahara wake kulingana na makubaliano yalivyo, pia waliambiwa kuna wakati amekuwa akisingizia majeraha, nalo wamemwekea, wakamwambia wakibaini hilo atapigwa faini, lingine ni kuchelewa mazoezini.
"Ameelezwa kuwa anatakiwa kuwa mfano kwa kuwahi mazoezini kila inapotakiwa, lakini jambo la nne ni kiwango, mabosi waligawanyika wakati wa kujadili dili hili, wakiamini kuwa kiwango chake kimeshuka, hivyo ameelezwa kuwa ni lazima aonyeshe kiwango cha juu kama anataka kuendelea kubaki Yanga baada ya mkataba kumalizika, nafikiri atasaini hivi karibuni kama halitatokea jambo lingine." kilisema chanzo hicho cha uhakika.