Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshahara unadaiwa kuwa tatizo marefa wa England

Anthony Taylor Denied Mwamuzi Anthony Taylor

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Waamuzi wa Ligi Kuu England wanalipwa mshahara kiduchu tofauti na wenzao wa ligi nyingine za Ulaya na hilo linawafanya wasafiri kwenda ng'ambo kutafuta mkwanja zaidi.

Waamuzi wa England wamekuwa gumzo kwa sasa baada ya kuboronga kwenye VAR katika mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Tottenham Hotspur na Liverpool. Mwamuzi, Darren England, aliyekuwa kwenye VAR, ambaye alishindwa kupitisha bao halali la Luis Diaz, ilielezwa hivi karibuni alikuwa huko Falme za Kiarabu kwenda kuchezesha mechi ili kupata malipo ya ziada.

Waamuzi wenye majina makubwa kama England, Anthony Taylor na Michael Oliver wanalipwa mishahara kuanzia Pauni 42,000. Kwa kila mechi wanalipwa posho ya Pauni 1,500 kama ni mwamuzi wa kati na wale wanaokuwa kwenye VAR, wanalipwa Pauni 850.

Kama mwamuzi atachezesha mechi 20 kwa msimu, basi atavuna Pauni 30,000, wakati kwa wale kwenye VAR, wakichezesha mechi 20, wanaweka mfukoni Pauni 17,000. Na hiyo inawafanya kukusanya kiasi cha jumla cha Pauni 89,000 kwa mwaka.

Huko Italia mshahara wa mwamuzi ni Pauni 48,000 na posho zao zipo juu, ambapo kwa kila mechi ni Pauni 3,300 – wakati wale watakaokuwa kwenye VAR wanalipwa Pauni 1,300. Akicheza mechi 20 kwa msimu, anavuna Pauni 66,000, wakati wa VAR analipwa Pauni 26,000. Hiyo ina maana kwa mwamuzi kwa mwaka anavuna hadi Pauni 140,000 – Pauti 51,000 zaidi ya kiwango kinacholipwa England.

Mshahara wa waamuzi La Liga ni Pauni 130,000. Kila mechi, mwamuzi wa kati analipwa Pauni 3,600 – hivyo atakuwa na uwezo wa kuvuna Pauni 72,000 endapo atachezesha mechi 20.

VAR kwenye La Liga analipwa Pauni 1,800 na kama atakuwa kwenye mechi 20, atapokea Pauni 36,000. Kwa ujumla, mshahara wa La Liga kwa mwaka ni Pauni 240,000 kwa mwamuzi wa kati – ikiwa ni Pauni 151,000 zaidi ya kiwango ambacho wanalipwa waamuzi wa Ligi Kuu England.

Chanzo: Mwanaspoti