Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mrithi wa Minziro apata jeuri mapema

Paul Nkataa Mrithi wa Minziro apata jeuri mapema

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata raia wa Uganda amesema baada ya kukitazama kikosi chake katika mechi mbili za kimataifa za kirafiki ameridhishwa na uwezo wa wachezaji na anaamini atafanya vizuri msimu huu kwenye Ligi Kuu.

Kocha huyo wa zamani wa Express na Villa SC za Uganda alitambulishwa Agosti 10, mwaka huu na Kagera Sugar akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’ ambaye mkataba wake umekwisha, kocha huyo yuko na timu hiyo katika ziara ya siku tano nchini Uganda.

Katika ziara hiyo ya kucheza mechi za kirafiki iliyoanza Agosti 9 hadi 15, mwaka huu, Kagera Sugar imeshacheza mechi mbili ikiichapa Wakisso Giants mabao 2-0 na sare ya 1-1 dhidi ya KCCA, huku ikiwatambulisha wachezaji watatu, Nassoro Kapama, Erick Mwijage na Emmanuel Charles.

Nkata alisema amejaribu kuwapa nafasi wachezaji wote ili waonyeshe uwezo na vipaji walivyonavyo na ameridhishwa na viwango vyao katika michezo hiyo, jambo ambalo linampa matumaini kuelekea Ligi Kuu.

“Mechi ya kwanza tulikuwa na uchovu wa safari lakini kizuri tulipata ushindi hiyo imeonyesha tukienda hivyo tunaweza kufaulu kwenye Ligi Kuu,nampa nafasi kila mmoja ili kupata timu nzuri kuliko msimu uliopita nashukuru kila mchezaji anaonyesha nia ya kupambana,” alisema Nkata

Akimzungumzia kocha huyo, Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabiti Kandoro, alisema ni kocha mwenye uzoefu wa miaka 20 na soka la Afrika akiwa amefundisha nchini Uganda na Kenya, muumini wa wachezaji wazawa na vijana, wana matumaini makubwa na yeye ya kufanya vizuri.

“Tumekubaliana kuwa kwenye nafasi zile za juu, tunaamini wachezaji wa ndani na vijana na yeye ana uwezo wa kuwasaidia vijana kuwa wachezaji wakubwa. Maono yake na yetu vinaendana ndiyo maana tumempa nafasi ya kuipeleka timu mbele,” alisema Kandoro.

Chanzo: Mwanaspoti