Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mrithi wa Mayele aipa jeuri Yanga

Joseph Guede Ds Mrithi wa Mayele aipa jeuri Yanga

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Yanga kinarudi tena mazoezini kambini Avic Town, huku kikijiandaa kumpokea straika mpya, Joseph Guede kutoka Ivory Coast, ambaye ameipa jeuri klabu hiyo inayoshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ikielezwa ataimarisha zaidi eneo la umaliziaji kikosini.

Guede amesajiliwa katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15 ili kuchukua nafasi ya Mghana Hafiz Konkoni aliyetolewa kwa mkopo Dogan Turk Birligi ya Cyprus, inaelezwa kuanzia leo ataungana na wenzake kambini.

Wakati akitarajiwa kuanza mazoezi na kuwa straika kinara wa kikosi hicho, Yanga inapata jeuri na kuamini kwamba Guede atafanya makubwa kwa kufunga mabao mengi kutokana na ubora wa wachezaji wanaomzunguka.

Guede anayecheza eneo la mshambuliaji wa kati (namba tisa), atakuwa akizungukwa na mafundi Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wanaocheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza katika eneo la viungo washambuliaji sambamba na winga mpya Augustine Okrah aliyeongezwa katika dirisha dogo sawa na Guede na mzawa, Shekhan Ibrahim aliyesajiliwa kutoka JKU ya Zanzibar.

Wachezaji hao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kupatikana kwa mabao ya Yanga ambapo Maxi, Pacome na Aziz Ki hadi sasa wamefunga jumla ya mabao 21 kwa pamoja, huku wakitoa jumla ya asisti sita, hivyo wamehusika moja kwa moja katika mabao 27 kati ya 31 yaliyofungwa na Yanga kwenye Ligi Kuu Bara baada ya mechi 11 kabla ya ligi kusimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na la Afrika (Afcon).

Kama Guede atatumia vyema ubora wa viungo hao sambamba na wachezaji wengine ambao ni wazuri kwenye kutengeneza nafasi akiwemo beki Kouassi Attohoula Yao mwenye asisti tano hadi sasa huenda kazi yake ya kucheka na nyavu ikawa nyepesi zaidi ndani ya kikosi hicho cha Wanajangwani.

Guede anaungana na Clement Mzize na Kennedy Musonda kwenye eneo hilo la ushambuliaji ambao nao wamechangia mabao saba, Mzize akifunga moja na kusisti matatu, huku Musonda akifunga mabao matatu.

WASIKIE MAKOCHA Kocha wa zamani wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kila klabu inasajili kutokana na matakwa ya benchi la ufundi hivyo ingizo jipya la nyota huyo ni imani kwake ataongeza ufanisi sehemu ya mwisho.

“Maana ya kuongezwa mshambuliaji maana yake kocha, Miguel Gamondi hakuridhika na waliopo sasa huu ni mtihani kwake wa kuonyesha hakusajiliwa kwa bahati mbaya ndani ya Yanga, kama atatuliza presha naamini atakuwa msaada mkubwa kwao,” alisema.

Nyota wa zamani wa timu hiyo, Sekilojo Chambua alisema usajili wa nyota huyo ni ishara tosha kwamba Hafiz Konkoni aliyeondoka alishindwa kabisa kuendana na kasi ya kikosi hicho hivyo tusubiri kuona ni kitu gani atakiongeza. “Mimi sijabahatika kumuona akicheza lakini mashabiki waache kumbebesha zigo nzito la kumfananisha na Fiston Mayele,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live