Kipa wa zamani wa Simba, Kelvin Mhagama amemuangalia kipa namba tatu wa timu hiyo, Ally Salim na kumwambia awe anatumia vyema nafasi za Aishi Manula na Ben Kakolanya kuwa timu ya taifa, Taifa Stars kufanya mambo ili ajihakikishe namba.
Salim ndiye aliyetumika kwenye mechi tatu za kimataifa za Simba, mbili zilizopigwa nchini Sudan dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na Al Hilal ya Sudan na jana ilipovaana na AS Arta Solar 7 wakati Manula na Kakolanya wakiwa na Stars iliyokuwa uwanjani jana kumalizana na Uganda katika mechi za kuwania Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan-2023).
Mhagama aliyewahi kuzichezea CDA, Mtibwa Sugar, Rayon Sport na Polisi za Rwanda alisema Salim anatakiwa kuonesha kwa vitendo uwezo alionao ili aendelee kubaki ndano ya timu hiyo.
“Hata mimi wakati nipo Simba kupata nafasi ilikuwa ngumu, kwani kulikuwa na makipa tofauti akiwamo Juma Kaseja, lakini ilipokuwa nikipata nafasi nilionyesha uwezo kweli kweli hadi unawaacha watu na maswali kwanini unakaa benchi,” alisema Mhagama.
“Yule kipa namba tatu (Salim) wakati ndio huu asibweteke nafasi aliyoipata ni kubwa, amejitahidi ila anatakiwa kukazana zaidi ya pale.”
Mhagama aliyewahi kuidakia Taifa Stars aligusia namna alivyokuwa Mtibwa na kuchuana na makipa hodari kama Steven Nemes na Ally Mohammed kuwania namba kikosini na kutoboa freshi.