Wakati wowote Tabora United itamtangaza kocha Denis Goavec kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi ya Goran Kopunovic ambaye mkataba wake umesitishwa mchana wa leo.
Mwanaspoti linafahamu tayari Goavec yuko mjini Tabora akisubiri kusaini mkataba wa mwaka mmoja na kuanza kazi muda wowote kuanzia sasa.
Klabu hiyo imetangaza kumalizana na Kopunovic leo Machi 21, 2024 baada ya makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba kutokana na matokeo mabovu kwenye Ligi Kuu Bara.
Kopunovic ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 21 za ligi akishinda nne, sare tisa na kupoteza nane akivuna pointi 21 akiiacha nafasi ya 13, huku akishinda mechi mbili za Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Nyamongo na Monduli Coffee na kuisaidia kutinga 16 Bora.
Licha ya Afisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwangala kueleza kwamba uongozi bado unaendelea kumsaka kocha mpya, lakini Mwanaspoti linafahamu Denis Goavec ndiye kocha mpya wa kikosi hicho.
Goavec raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 66 amekuwa na uzoefu na soka la Afrika akiwa na Leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA Pro Licence).
Kocha huyo amewahi kuifundisha pia JS Souara ya Algeria msimu wa 2014-2015 na timu ya taifa ya Benin mwaka 2010-2011, huku klabu yake ya mwisho kuifundisha ikiwa ni Cano Sport ya Guinea ya Ikweta Juni 30, 2020.
Kibarua cha kwanza cha Goavec akitua Tabora kitakuwa Aprili 4, mwaka huu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 16 Bora dhidi ya Singida Fountain Gate katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Tabora imebakiza mechi tisa dhidi ya JKT Tanzania, Kagera Sugar, Geita Gold, Mtibwa Sugar, Simba, Mashujaa, Ihefu, Yanga na Namungo.
Timu hiyo kwa sasa inaendelea kujifua na mechi za Ligi na Kombe la Shirikisho mjini Tabora chini ya makocha wasaidizi, Henry Mkanwa na Bernad Fabian wakisubiri kumpokea Goavec.