Miongoni mwa majina matakatifu ambayo hauwezi kuyakosa kwenye karatasi za vitabu vya soka la Tanzania ni jina la Mrisho Ngasa, miguu iliyobarikiwa utukufu wa kufanya kile anachopenda kufanya kwa usahihi mkubwa.
Bahati mbaya hakuzaliwa kwenye kizazi cha Azam Media na kilele nyingi mitandaoni, mara nyingi aliishia kuburudisha masikio ya wengi redioni, ni wachache tulipata bahati ya kushuhudia miujiza yake.
Nina mzungumzia mfungaji bora wa muda wote Taifa Stars, mchezaji pekee mzawa kubeba kiatu cha CAF Champion League akiwa kwenye ardhi ya nyumbani, binadamu aliyeshindwa kutenganisha hisia na soka, Mrisho Ngassa.
Hisia zilishinda vita ya kuongoza moyo wake, Ngassa alijipiga chapa ya Yanga kwenye paji la uso wake. Hakuweza kuishi vyema nje ya Yanga sababu ya kusujudu hisia zake.
Si Simba, wala Azam FC waliweza kutuliza hisia zake dhidi ya Yanga. Akiwa mchezaji wa Azam FC aliwahi kuvua jezi ya Azam uwanjani na kuvaa jezi ya Yanga, ni tukio la pili lisilosahaulika kwenye kumbukumbu za soka.
Tukio la kwanza ni ile ahadi yake, ndio aliwahi kuahidi nyumba yake ichomwe moto kama asingeifunga Simba, na aliweza kutimiza ahadi hiyo kwa vitendo. Ni dhahiri hisia zilishinda vita kwenye moyo wake.
Ni miguu iliyowahi kukanyaga Ulaya kabla ya miguu ya Mbwana Samatta, akiwa na Sounder Fc. Ngassa aliwahi kucheza dhidi ya Manchester United, akitokea sub.
Kwangu mimi Mrisho Ngassa anabaki kuwa mchezaji bora mzawa kuwahi kushuhudiwa kwenye ardhi ya Tanzania.