Mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo, George Mpole amesema huu ni wakati wa mshambuliaji wa Young Africans, Fiston Mayele kutamba na kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu kwa kuwa hakuna anayempa presha kwenye safu hiyo.
Mpole aliyetwaa tuzo hiyo msimu uliopita wakati anaitumikia Geita Gold FC akifunga mabao 17 na Mayele 16, amesema Mayele anakosa changamoto msimu huu kwa kuwa hakuna mshambuliaji mwingine anayefunga mfululizo kama ilivyokuwa akifanya yeye msimu uliopita.
“Niseme huu ni wakati wake Mayele, ukiangalia yeye na timu yake wako vizuri, lakini anaoshindana nao pia hawapo karibu kimagoli kwa hiyo ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo msimu huu tofauti na msimu uliopita tulivyokuwa tunachuana hatuachani.”
“Labda watu anaoshindana nao msimu huu hawampi changamoto, labda wangekuwa na nafasi au uwiano wa kufunga kila mechi wangeweza kumpa changamoto kama vile nilivyokuwa mimi nafunga mfululizo pamoja nilikuwa nipo timu ndogo,” amesema Mpole.
“Labda watu anaoshindana nao msimu huu hawampi changamoto, labda wangekuwa na nafasi au uwiano wa kufunga kila mechi wangeweza kumpa changamoto kama vile nilivyokuwa mimi nafunga mfululizo pamoja nilikuwa nipo timu ndogo,” amesema Mpole.
Mpole amesema hawezi kuzungumzia uwezo wa Jean Baleke aliyetua Simba SC Januari mwaka huu, akiwa amefunga mabao saba ya Ligi Kuu mpaka sasa, kwa kigezo cha mpira kutotabirika kwamba pengine mshambuliaji huyo angesajiliwa mwanzo wa msimu asingekuwa na moto alionao sasa.
Mayele anaongoza orodha ya wafungaji msimu huu kwa mabao 16 akifuatiwa na washambuliaji wa Simba SC, Moses Phiri na Saido Ntibazonkiza waliofunga mabao 10 kila mmoja.