Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpo? Dabo anawachora tu Yanga

Dabo Azam 128.png Mpo? Dabo anawachora tu Yanga

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga kuna sapraizi yenu kwa kocha wa Azam, Youssouph Dabo ambaye licha ya kukiri ubora wa Wananchi hasa katika safu ya ushambuliaji, amedai kuwa na kundi la mastaa wenye uwezo wa kukabiliana na vijana hao wa Miguel Gamondi.

Dabo ambaye alitua nchini mwishoni mwa msimu uliopita ili kusoma mazingira mapya ya kazi kabla ya kutambulishwa, bado hajapoteza mchezo Ligi Kuu Bara na ameiongoza timu hiyo kushinda michezo minne na sare moja, hivyo imekusanya pointi 13 zilizoifanya kuwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo unaoongozwa na Simba yenye pointi 15.

Hii ni tofauti na Yanga ambayo haijatoka sare, lakini imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Ihefu, hivyo hali hiyo inafanya mchezo wa kesho kati ya Yanga na Azam kuwa mkali zaidi.

Akiwa Chamazi yalipo maskani ya Azam FC, Mwanaspoti ambalo ni gazeti bora la michezo Tanzania, lilitia timu siku chache zilizopita na kufanya mahojiano na kocha huyo ambaye anaamini vijana wake wana nafasi ya kuisapraizi Yanga.

“Itakuwa mechi ya timu mbili kubwa. Najua ni mechi ambayo pia itakuwa ikifuatiliwa na wengi kutokana na mpira wa Tanzania kukua siku baada ya siku. Natamani kuona kila upande ukiwa sawa ili mpira uchezwe. Tunajua pamoja na ubora walionao wanao upungufu wao,” anasema kwa kujiamini.

Mara ya mwisho kwa Yanga na Azam FC kukutana ilikuwa mwanzoni mwa msimu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambako Wananchi walishinda mabao 2-0.

KILA MECHI NGUMU

Katika mechi tano alizoiongoza Azam FC ameshinda dhidi ya Tabora United mabao 4-0, Tanzania Prisons 3-1, Singida Big Stars 2-1, Dodoma Jiji 0-0 na Coastal Union 1-0, lakini Dabo anasema ligi ya ni ngumu kutokana na ushindani uliopo.

“Ligi ya Tanzania ni ya ushindani. Nimeona kwenye michezo ambayo tumecheza naamini ushindani utaendelea kuongezeka raundi zinazofuata. Tulipata upinzani mkubwa dhidi ya Dodoma Jiji na dhidi ya Coastal,” anasema kocha huyo.

Pamoja na kuwa timu yake kwenye michezo mitano imefunga mabao 10 huku ikiruhusu mawili, Dabo anasema amevutiwa na mshambuliaji mmoja wa Coastal Union ambaye alishindwa kumtambua kwa majina, lakini akamtaja kwa nafasi yake.

“Kuna mshambuliaji mmoja wa kati wa Coastal ni mchezaji ambaye amenivutia mpaka sasa kwenye ligi nje ya wachezaji ambao nipo nao kwenye kikosi changu. Ana kasi, nguvu na maarifa nimekuwa nikipenda aina yake ya uchezaji,” anasema.

SOKA LAKE

Dabo anajitanabaisha kama kocha anayependa mchezaji mwenye nidhamu, upambanaji na kufuata maelekezo yake.

“Mchezaji mwenye sifa hizo anaweza kuwa sehemu ya mipango yangu. Hakuna kocha ambaye hapendi kuona timu yake ikicheza soka la kuvutia na kupata matokeo mazuri. Napenda kuwa na timu yenye uwezo wa kushambulia na kuzuia kwa pamoja,” anasema kocha huyo anayependa kutumia mfumo wa 4-2-3-1 na muda mwingine hubadilika na kutumia 4-4-2.

UBORA WA KIKOSI

Licha ya kuendelea kukisuka kikosi, Dabo anafurahishwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ambao wamekuwa wakiuonyesha kuanzia mazoezini.

“Kuwa na wachezaji wengi ambao kila mmoja anapambana kupata nafasi ni jambo zuri.Ambacho nimekuwa nakifanyia kazi ni staili nayotaka kuona kila mchezaji ikiwa kichwani mwake kulingana na nafasi ambayo atatakiwa kutumika,” anasema.

KUHUSU UBINGWA

Kwa namna ambavyo wameuanza msimu, kochahuyo an-aamini Azam FC inaweza kutoa changamoto dhidi ya Simba na Yanga kwenye mbio za ubingwa. “Tunatakiwa kuendelea kufanya vizuri kwenye kila mchezo. Ligi ni kama mbio za marathoni huwa na vipindi vizuri na vigumu. Kama timu tunatakiwa kushikamana ili kufanikisha kile ambacho tumedhamiria. Kwangu naona nafasi ipo tena kubwa kutokana na aina ya wachezaji nilionao,” anasema kocha huyo.

VIWANGO VYA WAZAWA

Sospeter Bajana na Feisal Salum ni miongoni mwa mastaa wazawa ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Dabo, anayeeleza juu ya Tanzania kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji.

“Hapo kabla sikuwahi kabisa kujua kuhusu ubora wa wachezaji wa Kitanzania kwa kiwango kikubwa, lakini wakati nikiwa hapa nimejionea. Ni kama ilivyo katika mataifa mengine ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika ambako mpira unaonekana kupiga hatua kubwa,” anasema kocha huyo.

“Uwepo wa wachezaji wazawa ukiongeza na majina machache ya kigeni ni wazi kuwa timu inaweza kuwa katika hatua nyingine naamini kuwa Tanzania ni nchi yenye vipaji na sio ajabu hata kuona ikifanya vizuri kwenye fainali zijazo za Afcon.”

MABADILIKO YA NAHODHA

Dabo anasema ni mabadiliko ya kawaida kutokea kwenye timu kwa sababu hata msimu uliopita nahodha mkuu alikuwa Bruce Kangwa ambaye kwa sasa hayupo na Sospeter Bajana alichukua mikoba yake na yeye kama kocha aliamua kufanya mabadiliko mengine kwa ajili ya kuleta ufanisi zaidi.

“Bajana bado ni kiongozi wa wachezaji niliamua kumpa kitambaa Daniel Amoah ili kuleta ufanisi kwa sababu hata wao niliwaelezea kuwa ana karama ya uongozi na ataweza kusimama kwa ajili kuwa kiunganishi kati ya uongozi na wachezaji hii haimanishi kuwa Bajana hastahili ila yeye bado ni kiongozi wa wachezaji wenzake na wanampenda,” anasema Dabo.

NIDHAMU YA WACHEZAJI

Dabo anasema kuwa amekuwa akiwaambia wachezaji wake kuwa lazima wajitambue kuwawapo kwao kwenye timu ya Azam ni kwa manufaa yao na hakuna mtu anapaswa kuwakumbusha kuhusu masuala ya nidhamu hivyo basi inabidi wajitambue kabla ya kusukumwa kufanya majukumu yao.

“Kila mmoja anajua yupo kwa nini Azam hakuna mtu anaepaswa kuwakumbusha kwani wote ni watu wazima niliwaambia wanapaswa wakue kiakili kwa kuweza kufuata masharti yaliyopo ili kuepusha misuguano isokuwa ya lazima ingawa wakati naanza ilikuwa ngumu wao kunielewa kwa sasa wanajua mfano wakichelewa wanakutana na penati za kukatwa fedha” anasema Dabo.

BONASI KUKATWA

Licha ya kucheza vizuri na kuambulia sare dhidi ya timu ya Dodoma wachezaji wa Azam walilalamikia ishu ya kutokupewa bonasi ya mchezo huo ambapo kocha Dabo alitoa ufafanuzi kwa kusema kuwa hiyo sio mara ya kwanza kwani hata msimu uliopita walifanyiwa hivyo.

“Hata msimu uliopita ilikuwa ni hivyo na baadhi ya watu wanaamini kuwa mimi ni mgumu lakini mimi niko karibu sana na wachezaji na naongea nao tunapokubaliana kitu lazima tuheshimu makubaliano na matokeo ni yetu sote kwa ligi ni kama mbio lazima tupambane mpaka mwisho wa msimu,”alisema Dabo.

Chanzo: Mwanaspoti