Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpo? Afcon 2023 kutikisa Ligi Kuu England

Salah Vs Malawi Mpo? Afcon 2023 kutikisa Ligi Kuu England

Wed, 20 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Fainali za Mataifa ya Afrika 2023 zinatarajiwa kuvuruga msimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku baadhi ya klabu za Ligi Kuu ya England zikitarajiwa kuathirika pakubwa.

Katika kujaribu kuzuia mwingiliano wa ratiba ya msimu kwa klabu nyingi za Ulaya, fainali za Mataifa ya Afrika 2023 zilipangwa kuchezwa Juni na Julai. Hata hivyo, kutokana na wasiwasi wa hali mbaya ya hewa nchini Ivory Coast, michuano hiyo ilirudishwa nyuma. Sasa itaanza kati ya Januari 13 hadi Februari 11.

Kwa miaka mingi, moja ya mitego ya kusajili wachezaji bora wa Kiafrika imekuwa na matarajio ya kuwapoteza wakati wa msimu wa baridi.

Na kutokana na mabadiliko ya ratiba, msimu huu hautakuwa tofauti. Ni klabu chache za England ambazo zitaepuka madhara ya AFCON 2023, huku wachezaji wapatao 43 wakiwa katika tishio la kukosa michezo ya klabu zao wakati michuano hiyo itakapoanza kutimua vumbi mwaka mpya.

Hawa ni baadhi ya nyota wa Ligi Kuu England ambao wanaweza kukosekana kwenye klabu zao kutokana na majukumu ya kitafita ambayo watakuwa nayo.

Said Benrahma (Algeria)

Benrahma amekuwa mhimili mkuu wa timu ya West Ham tangu kuhama kwake kutoka Brentford majira ya joto 2020. Alifunga bao katika fainali ya Ligi ya Europa Conference msimu uliopita na atakosekana kwa The Hammers atakapotimkia Ivory Coast.

Rayan Ait-Nouri (Algeria)

Ait-Nouri ni jina jipya kwenye kikosi cha Algeria, baada ya kuipiga chini Ufaransa Machi 2023. Wolves itawabidi kutafuta njia mbadala ya wao kuendelea na maisha bila ya nyota huyo.

Bertrand Traore (Burkina Faso)

Kiwango cha Traore kimekuwa cha kupanda na kushuka tangu ajiunge na Aston Villa. Maendeleo yake yalitatizwa na kampeni ya msimu wa 2022-23, na atakuwa na matumaini ya kurejea katika ubora wake kwa klabu na nchi katika miezi michache ijayo.

Dango Ouattara (Burkina Faso)

Ouattara alikuwa mmoja wa wachezaji waliosajiliwa Januari ambao waliisaidia Bournemouth kusalia kwenye Ligi msimu uliopita. Kwa bahati mbaya, jeraha limezuia kuhusika kwake hadi sasa katika kampeni hii, ingawa muda wowote anaweza kurejea na kuendeleza moto wake.

Issa Kabore (Burkina Faso)

Kabore hajanusa kikosi cha kwanza tangu ajiunge na Manchester City 2020, lakini ikiwa atafanya vizuri katika klabu mpya ya Luton Town, Pep Guardiola kumjumuisha kwenye mipango yake. Luton itabidi kufikiria maisha mapya bila mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22.

Bryan Mbeumo (Cameroon)

Huku Ivan Toney akitumikia adhabu ya kusimamishwa kwa kukiuka sheria za kamari, shinikizo lilikuwa kwa Mbeumo mwanzoni mwa msimu. Mcameroon huyo amefanikiwa licha ta kuwa chini ya uangalizi,amekuwa na mwanzo mzuri wa msimu akiwa na Brentford.

Andre Onana (Cameroon)

Baada ya mzozo wa hali ya juu na kocha wa Cameroon Rigobert Song kuhusu mfumo wa uchezaji wa timu hiyo uliomfanya aondoke kwenye Kombe la Dunia mapema, Onana alirejea kwenye kikosi cha kimataifa Septemba. Aliisaidia timu hiyo kupata nafasi ya kufuzu kwa AFCON 2023. Manchester United tayari imeanza hesabu za maisha bila ya kipa huyo namba moja kwenye kikosi chao.

Yoane Wissa (DR Congo)

Sawa na Mbeumo, Wissa amekuwa na jukumu la ziada la kufunga mabao lililowekwa mabegani mwake bila kuwepo Toney. Yeye pia yupo chini ya uchanguzi, na DR Congo itakuwa na matumaini kuwa anaweza kuwa na mchango kwenye kikosi chao katika AFCON.

Pelly Ruddock Mpanzu (DR Congo)

Ruddock Mpanzu amefurahia kupanda kwa Luton kwani moja ya ndoto zake ilikuwa ni kucheza Ligi Kuu England. Kucheza kwenye AFCON ya 2023 na nchi yake itakuwa ni hatua nyingine kwake.

Mohamed Elneny (Misri)

Elneny alitarajiwa kuondoka Arsenal katika majira ya joto kutokana na kukumbana na changamoto ya namba lakini alibadili maamuzi na kuamua kuendelea kupigania nafasi kwenye kikosi hicho. Kama hatoendelea kucheza anaweza kuwa na wakati mgumu kuitwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ila uzoefu unaweza kufanya afikiliwe mara mbilimbili wakati wa uchaguzi wa wachezaji.

Mohamed Salah (Misri)

Salah yuko tayari kukosa mechi za Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth, Chelsea na Arsenal ikiwa Misri itafanya vyema msimu huu wa baridi. Hata hivyo, hili linaweza kuwa tatizo la Al-Ittihad, huku timu hiyo ya Saudi Pro League ikidhamiria kumsajili fowadi huyo kwa ada ya rekodi ya dunia.

Thomas Partey (Ghana)

Ujio wa Declan Rice na Kai Havertz msimu wa joto ulionekana kutishia nafasi ya Partey kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal, haswa baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022-23. Lakini Arteta amekuwa na imani na nyota huyo wa Ghana ambaye bila shaka atarejea kwenye safu ya kiungo ya Black Stars.

Antoine Semenyo (Ghana)

Semenyo hajaanza kuonyesha makali yake tangu ajiunge na Bournemouth kutoka Bristol City ya Championship Januari iliyopita, alifunga mara moja pekee msimu wa 2022-23. Uchezaji wake umetosha kumfanya mara kwa mara kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa la Ghana.

Tariq Lamptey (Ghana)

Baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hadi ikabidi Brighton kuingia sokoni kumsajili kiraka James Milner, anaonekana kuwa sawa kwa sasa na amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho. Kocha wa Ghana Chris Hughton amekuwa akivutiwa na uchezaji wake.

Jeffrey Schlupp (Ghana)

Kwa kushangaza Schlupp aliachwa nje ya kikosi cha Black Stars kwa Kombe la Dunia 2022, ni kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa ambaye amekuwa akifanya vizuri akiwa na Crystal Palace.

Jordan Ayew (Ghana)

Ayew alisifu "uzuri wa soka" baada ya Ghana kufuzu AFCON kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Fowadi huyo mzoefu wa Crystal Palace anaweza kubebeshwa jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya Black Stars ni kati ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi kwenye kikosi hicho.

Mohammed Kudus (Ghana)

West Ham walifanya vyema kumnasa Kudus msimu huu wa joto, huku baadhi ya klabu kubwa barani Ulaya zikimfuatilia katika miaka michache iliyopita. Kwa sababu ya kuchelewa kuwasili, mashabiki wa Hammers bado hawajaona kilichobora kutoka kwake.

Hamed Traore (Ivory Coast)

Hapo awali alisajiliwa kwa mkopo kutoka Sassuolo, Traore alijiunga jumla na Bournemouth msimu wa joto na kocha Andoni Iraola amekuwa akimsifu raia huyo wa Ivory Coast. Ushindani wa nafasi za mbele ni mkali katika timu yake ya taifa, lakini anaweza kuwa na nafasi ya kulitumikia taifa lake.

Simon Adingra (Ivory Coast)

Adingra ni kati ya wachezaji vijana ambao wanafanya vizuri kwenye kikosi cha Brighton. Aliponunuliwa kwa pesa kidogo kutoka Nordsjaelland, nyota huyo alipelekwa kwa mkopo Union SG msimu uliopita na sasa amerejea Amex.

Amad Diallo (Ivory Coast)

Huku Manchester United ikionekana kuwa butu kwenye safu yao ya ushambuliaji msimu huu wa 2023-24, Amad ana nafasi nzuri ya kucheza kwa Mashetani hao Wekundu mara atakaporejea katika utimamu kamili. Pia ameichezea Ivory Coast mechi nne tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 2021.

Maxwel Cornet (Ivory Coast)

Mchezaji mwingine wa West Ham ambaye huenda akakosekana kwenye kikosi hicho kwa ajili ya AFCON ni Cornet, ambaye ana uhakika wa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha timu yake ya taifa.

Ibrahim Sangare (Ivory Coast)

Sangare anaonekana kuwa chaguo bora kwa Nottingham Forest tangu ajiunge nayo akitokea PSV ya Uholanzi. Akiwa na Ivory Coast hadi sasa nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 amecheza mechi zaidi ya 30.

Serge Aurier (Ivory Coast)

Aurier amekuwa katika kiwango bora tangu kuanza kwa msimu wa 2023-24, beki huyo wa pembeni alitoa pasi ya bao kwenye mchezo dhidi ya Sheffield United katika ushindi muhimu ambao Forest iliupata wa mabao 2-1. Atakuwa mmoja wa wachezaji wenye uzoefu zaidi katika kikosi cha Ivory Coast.

Willy Boly (Ivory Coast)

Boly alichelewa kuwa sehemu ya kikosi cha timu yake ya taifa, hakucheza mechi yake ya kwanza ya Ivory Coast hadi 2020 akiwa ameiwakilisha Ufaransa katika ngazi ya vijana. Yeye si beki wao wa kati chaguo la kwanza pia, jambo ambalo liweza kuwafadhaisha zaidi Forest ikiwa ataishia kusafiri kwa ajili ya AFCON 2023.

Cheick Doucoure (Mali)

Akihusishwa na kuhamia Liverpool msimu huu wa joto, Doucoure aliishia kusalia Crystal Palace jambo lililowafurahisha mashabiki wa klabu hiyo. Katika habari mbaya zaidi kwa mashabiki wa Eagles, Roy Hodgson anatazamiwa kutokuwa na kiungo wake wa kati kwa kipindi chote ambacho Mali itashiriki katika dimba hilo.

Ismaila Coulibaly (Mali)

Coulibaly alitajwa kuwa anaweza kuwa mchezaji mkubwa sana miaka michache ijayo alipowasili Bramall Lane mwaka wa 2020. Baada ya kwenda kwa mkopo Beerschot ya Ubelgiji kwa miaka miwili, alirejea Sheffield United na kuanza kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Yves Bissouma (Mali)

Mmoja wa wanufaika wengi wa uteuzi wa Ange Postecoglou kama kocha wa Tottenham msimu wa joto, Bissouma ameanza vyema msimu huu. Amekuwa kwenye kiwango bora sana lakini kocha huyo itabidi atafute mpango mbadala kwani huenda akakosa huduma ya kiungo huyo.

Boubacar Traore (Mali)

Traore alifanya vizuri akiwa na Wolves kiasi cha kujipatia mkataba katika klabu hiyo kufuatia kipindi cha kwanza cha mkopo msimu uliopita kumalizika. Hata hivyo, anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha Mali.

Nayef Aguerd (Morocco)

Aguerd amekuwa akivutia klabu nyingi za Ligi Kuu England hivi karibuni, jambo ambalo ni dhihirisho la mwanzo wake mzuri wa maisha akiwa West Ham wakati wa kampeni za 2022-23. The Hammers hawakuwa na wachezaji bora zaidi katika safu ya beki wa kati hadi kusajiliwa kwa Konstantinos Mavropanos msimu huu wa joto, mpango ambao huenda ulichangiwa na uwezekano wa kutokuwepo kwa Aguerd ambaye anaenda AFCON.

Anass Zaroury (Morocco)

Zaroury hakuianza vyema kazi kwenye Ligi Kuu England, kwa kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja wakati wa mechi ya ufunguzi wa pazia la timu yake dhidi ya Manchester City. Anahitaji kuonyesha kiwango bora zaidi kabla ya kikosi cha Morocco kuchaguliwa huku ushindani wa nafasi ukiwa mkali.

Alex Iwobi (Nigeria)

Baada ya kuiwakilisha England katika soka la vijana, Iwobi alibadili uamuzi na kuichezea Nigeria mwaka 2015 na tangu wakati huo amekuwa tegemeo kwa Super Eagles. Watakuwa na matumaini kwamba kuhamia kwake Fulham kunathibitisha kuwa alifanya uamuzi wa busara baada ya kuwa na wakati mgumu akiwa Everton.

Taiwo Awoniyi (Nigeria)

Nguvu ya Nigeria katika safu yake ya ushambuliaji ni kubwa. Kucheza washambuliaji wawili ni nadra katika soka la kiwango cha juu siku hizi, lakini unapokuwa na wachezaji kama Victor Osimhen, Kelechi Iheanacho, Samuel Chukwueze, Gift Orban na Awoniyi kuchagua unaweza kufanya hivyo. Awoniyi amekuwa akifanya vizuri akiwa na Nottingham Forest.

Ola Aina (Nigeria)

Akianzia soka lake akiwa Chelsea, Aina alichukua uamuzi wa kijasiri wa kujiunga na Torino mwaka wa 2019. Baada ya kuonja kushuka daraja akiwa mkopo katika klabu ya Fulham wakati wa kampeni za 2020-21, atakuwa na matumaini ya kupata nafasi ya kufanya vizuri kwa sasa akiwa na Nottingham Forest na timu yake ya taifa.

Nicolas Jackson (Senegal)

Uhamisho wa Jackson kwenda Chelsea akitokea Villarreal majira ya kiangazi haukutarajiwa, ndiye mshambuliaji anayetegemewa na Mauricio Pochettino kutokana na Christopher Nkunku kuwa majeruhi, itawabidi matajiri hao wa London kuwa na mpango mbadala wakati wa AFCON.

Idrissa Gueye (Senegal)

Kumekuwa na minong'ono kwamba Gueye anaweza kustaafu soka la kimataifa, lakini alipinga vikali tetesi hizo hivi karibuni. Si habari njema kwa Everton ambao wanahitaji wachezaji wao wote bora wapatikane mara nyingi iwezekanavyo kwani wanatazamia kupambana tena na janga la kushuka daraja msimu huu.

Cheikhou Kouyate (Senegal)

Mchezaji muhimu katika ushindi wa Senegal wa AFCON 2021, Kouyate anajivunia takriban mechi 300 za Ligi Kuu ya England akiwa na West Ham, Crystal Palace na Nottingham Forest. Ana umri wa miaka 33 sasa, lakini anasalia kuwa mtu muhimu kwa klabu na nchi yake.

Pape Matar Sarr (Senegal)

Sarr alilazimika kuwa mvumilivu kwa nafasi yake ya kikosi cha kwanza msimu uliopita licha ya kiwango kibovu cha Tottenham. Yeye ni miongoni mwa wachezaji wanaoaminika zaidi wa Postecoglou.

Chanzo: Mwanaspoti