Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango ataka timu za JKT izipiku Simba, Yanga

IMG 4505.jpeg Mpango ataka timu za JKT izipiku Simba, Yanga

Sat, 1 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa,(JKT) kuongeza msukumo katika kuibua,kukuza na kuendeleza vipaji huku akizitaka timu za Mashujaa na JKT Tanzania kuleta ushindani kwa Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.

JKT ina timu mbili,Mashujaa na JKT Tanzania ambazo zitashiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao mara baada ya kufanya vizuri katika Championship iliyomalizika hivi karibuni huku kwa upande wa wanawake wakiwa na timu ya JKT Queens ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya soka ya Wanawake (WPL)

Dk Mpango ameyasema hayo Jumamosi Julai Mosi, 2023 wakati akizindua maonyesho ya jeshi hilo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake yatakayofikia kilele chake Julai 10,2023 katika viwanja vya Jamuhuri.

Amesema watanzania walio wengi wanapenda kuona timu za JKT zinafanya vizuri katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu hata kuzipiku timu za Yanga na Simba.

“Lakini tufanye vizuri katika michezo mingine kama mpira wa miguu, pete kwa ajili ya wanawake, riadha na kadhalika,naamini JKT inaweza katika kukuza michezo muziki, sanaa na utamaduni,”amesema Dk Mpango Hata hivyo amelitaka Jeshi hilo kuongeza msukumo katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema wanaendelea kujipanga kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendeleza na kuibua vipaji.

“Kabla ya Bunge tulikubaliana na dada yangu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (Pindi Chana) na Makatibu wakuu wawili wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na watalaam kuchambua maeneo mahususi ambayo wizara hizi mbili zinaweza kushirikana,”amesema Waziri Bashugwa.

Mkuu wa JKT Meja Jenerali, Rajabu Mabele amesema katika kuelekea maadhimisho hayo watakuwa na mabonanza mbalimbali yatakayoshirikisha mpira wa wavu na kikapu.

Amesema bonanza hilo limetanguliwa na mbio za JKT marathoni zilizofanyika Juni 25, mwaka huu katika uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma.

Chanzo: Mwanaspoti