Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moussa Diaby ameona mambo yasiwe mengi

Moussa Diaby DD Moussa Diaby

Sat, 3 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Utaamua unachotaka katika maisha. Na wakati mwingine ukitaka kumuua nyani usimtazame sana usoni. Rafiki yetu Mfaransa Moussa Diaby ameamua kutomuangalia sana nyani usoni. Katika mfano huu mgeuze nyani kuwa maisha yako ya kawaida.

Yeye hatakuwa wa kwanza na wala hawezi kuwa wa mwisho. Diaby alitua England msimu mmoja uliopita akitokea Bayer Leverkusen. Aliamua kuvaa jezi ya Aston Villa, ingawa alikuwa anatamaniwa na wakubwa wengi. Chelsea, Arsenal, Manchester United na wengineo. Sijui ilikuwaje akaamua kwenda zake kwa Unai Emery. Villa walilipa pesa ndefu kidogo kuinasa saini yake.

Baada ya miezi 12 tu klabuni, Diaby ametangazwa kuwa mchezaji mpya wa Al-Ittihad ya Saudi Arabia. Ameona mambo yasiwe mengi. Ndio, yasiwe mengi. Kuna mastaa wengi wamehalalishwa kwenda Saudi Arabia kuchuma pesa za utajiri wa mafuta. Wale ambao wanapitisha miaka 30. Au wale ambao wanaonekana kuozea benchi. Hawa wengi wao huwa hawaoni aibu kufuata pesa za mafuta pale Saudia.

Lakini kuna wale ambao hawajafikisha umri huo. Wengi huwa wanaona aibu kwenda Saudia. Kuna wale ambao mioyo haiwatumi. Kuna wale ambao wanataka kushinda mataji na kutangaza majina kwa ukubwa zaidi Ulaya ili historia zao zikumbukwe kwa urahisi zaidi. Haijalishi umetwaa mataji mangapi Saudi Arabia hauwezi kukumbukwa kama ulikuwa mwanasoka mahiri ulimwenguni.

Saudia ni kama Afrika tu au vilevile ni kama ilivyo Amerika Kusini kwa sasa. Unaweza kuamua kucheza huko na ukashinda mataji yako 27, lakini usichukuliwe kama mchezaji mahiri uliyeacha kumbukumbu kama haujacheza Ulaya ukachukua Ligi Kuu England, Hispania Italia na nyinginezo. Ukachukua Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ukachukua hata UEFA. Kisha ukarudi nchini kwako kutwaa Kombe la Dunia, Euro au Copa America.

Halafu sasa kuna mchezaji kama Diaby. Hajali chochote. Wakati Watanzania wakisheherekea Sikukuu ya Sabasaba mwaka huu, yeye ndio kwanza alikuwa anatimiza miaka 25. Kijana mbichi na mwenye kipaji kikubwa. Alichoangalia kwa haraka haraka ni mshahara mnono ambao atalipwa Saudi Arabia. Basi. Mengineyo hajali sana.

Msimu wake wa kwanza England hakung'ara sana. Ni kitu cha kawaida kwa wachezaji wengi. Katika ligi ngumu kama ya England huwa wanahitaji muda wa kuzoea ligi (adoption period). Msimu wa pili ulitazamiwa Diaby awe wa moto kwa ajili ya kuanza kusaka safari ya kwenda Liverpool, Barcelona, Bayern Munich, Chelsea, Manchester United, Manchester City, Arsenal na kwingineko.

Yeye ameona mambo yasiwe mengi. Hakukuwa na muda wa kusaka timu kubwa na wala hakukuwa na muda wa kusaka mataji na kutangaza jina kubwa, na wala hakukuwa na muda wa kuisaka miaka 30 ilipo. Amechukua chake mapema kabisa. Amenikumbusha rafiki yetu wa zamani, Oscar. Yule staa wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil. Oscar dos Santos Emboaba JĂșnior maarufu Oscar hakutaka kuwa mnafiki.

Aliweka wazi namna ambavyo amekulia katika umaskini mkubwa kwao Brazil na namna ambavyo ana kundi kubwa la watu lililo nyuma yake na linamtegemea katika maisha ya kila siku. Diaby hajakulia katika maisha ya Oscar, lakini ameamua kuchukua chake mapema.

Kwa sasa safari ya kucheza Saudia imekuwa kama mtego kwa wachezaji. Namna ambavyo watakavyoonekana katika jamii. Ni safari ambayo pia wanasoka wanapimwa uwezo wao wa kiushindani katika mioyo yao. Mpira mwepesi halafu pesa nyingi. Lakini hapo hapo wanapimwa kwa kile ambacho wanakifikiria katika timu za taifa. Ligi ya Saudia bado haipo tayari sana kumuandaa mchezaji kucheza soka la kishindani na kuwania namba vilivyo katika kikosi cha timu ya taifa.

Inatokea nadra kwa mchezaji kama Ng'olo Kante kufanya vizuri katika umri ule halafu akiwa anatokea Saudia huku akiwa anacheza katika moja kati ya mataifa makubwa katika soka duniani. Kama unacheza taifa kama Ukraine, Poland au Austria, basi unaweza tu kuendelea kuichezea timu ya taifa kama ulienda huko ukiwa na jina kubwa baada ya kutamba Ulaya. Lakini ni wazi kwamba nafasi yako kama ina ushindani kutoka kwa mastaa wanaocheza England, Ujerumani, Hispania, Italia na Ufaransa basi kocha atawapendelea wachezaji wa Ulaya kuliko wa Saudia.

Stori za kwamba Saudia inaelekea kuwa na ligi kali kama ilivyo ligi hizi tano barani Ulaya ni za mtaani tu na za wachezaji waliokimbilia pesa Saudia wanaojaribu kujifariji kwamba wanapata pesa na kucheza katika ligi ngumu. Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa mastaa ambao nimewahi kuwasikia wakitudanganya kutoka Saudia.

Diaby hakutaka kuangalia nafasi yake katika kombe lijalo la dunia. Ameamua kuchukua chake mapema. Alikosa kwenda Euro na sasa kuna asilimia kubwa atakosa kwenda Marekani, Canada na Mexico katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia 2026. Hili lipo wazi. Kuna mastaa wengi wa Kifaransa wanaotamba Ulaya.

Nadhani inaweza pia kuwa mwanzo wa fasheni kwa wanasoka kadhaa ambao watataka kucheza Saudia kwa miaka michache kisha warudi tena Ulaya. Swali ni kama wataweza kurudi Ulaya na kucheza kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa awali. Sidhani kama inaweza kuwa hivyo. Yannick Carrasco aliwahi kutukimbia Ulaya akaenda zake kuchuma pesa za Wachina. Alirejea Ulaya akiwa mchezaji wa kawaida. Kasi ikamtupa mkono.

Hadi sasa sijui kama ninamlaumu Diaby au ninampongeza. Ni uamuzi wake. Nimeelezea tu namna ambavyo amechukua chake mapema pengine kuliko wale ambao niliwatazamia kwenda Saudi Arabia katika dirisha hili. Nilitazamia kwamba Mo Salah na Kevin De Bruyne wangeweza kufungasha virago mapema kuliko yeye na kwenda Saudia. Hata hivyo amewahi mapema kwa kasi ya umeme.

De Bruyne ametimiza miaka 33 wakati Salah amepitisha 30. Wameshinda kila kitu na hakuna anayewadai kwa lolote katika ngazi za klabu. Hata hivyo, Diaby ameamua tu kuwawahi. Hataki mambo mengi katika maisha yake ya soka na nadhani anataka kukumbukwa kwa noti ambazo amechuma katika soka kuliko kukumbukwa kwa mataji binafsi na mambo mengineyo.

Waarabu wasije wakatupa 'surprise' tu kwa kuweza kuwanyakua wachezaji kama Bukayo Saka, Vinicius Junior, Rodrigo, Lamine Yamal, Nico William, Kobbie Mainoo na wengineo wa umri huu. Watakuwa wametuvunja maini. Tunahitaji wachezaji kama hawa kwa ajili ya mechi kali za soka pale Ulaya. Sawa, Mwarabu ana pesa za kufanya chochote kwa haya, lakini angetupumzisha kidogo.

Unapohisi kwamba katika hao huenda kuna wachezaji wenye moyo kama wa Diaby unaingiwa na wasiwasi kidogo. Wanasoka wenyewe wa siku hizi hawaeleweki. Kuanzia wao hadi mawakala akili zao ziko katika pesa zaidi. Wengine hadi wazazi wao akili zao zipo katika pesa zaidi na hawajali sana kuhusu maendeleo ya watoto wao.

Mungu alitunusuru kwamba pesa zao hazikutumika katika staili hii wakati tulipokuwa tunashuhudia ubora wa kina Zinedine Zidane, Ronaldinho Gaucho, Rui Costa, Paul Scholes na wengineo kibao. Si ajabu tusingeshuhudia ubora wao hadi mwisho kama kina Al-Ittihad wangeanzisha utaratibu huu wakati huo. Shukrani tuliona ubora wao mpaka mwisho.

Lakini kwa sasa tumeanza kuishi kwa mashaka. Ukisikia kina Al-Ittihad wanamtaka Saka unajua lolote linawezekana. Inategemea tu akili ya mchezaji na watu wanaomzunguka. Shukrani kwa watu waliomzunguka Kylian Mbappe wakati ule alipopewa ofa ya ubilionea juu ya ubilionea alipokorofishana na PSG. Lakini tuna watu kama Moussa Diaby. Wanamuua nyani usoni.

Chanzo: Mwanaspoti