Jose Mourinho ameripotiwa kuwa kwenye hatua nzuri ya kupata kazi mpya itakayomrejesha kwenye soka, imeelezwa.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United amekuwa hana kazi tangu alipofutwa kazi na AS Roma, Januari mwaka huu, miezi minane baada ya kuiongoza timu hiyo kubeba Europa Conference League.
Mourinho, 61, amehusishwa na kazi kadhaa kwa kipindi cha miezi minne tangu alipofukuzwa huko AS Roma, huku miongoni mwa timu alizohusishwa ni pamoja na kurudi Old Trafford.
Kwa mujibu wa SportItalia, Mreno huyo yupo kwenye hatua nzuri ya kujiunga na Al-Qadisiyah ya Saudi Arabia. Lakini, shida ni Mourinho havutiwi na mpango wa kwenda Saudi Pro League.
Madai ni Mourinho yupo kwenye dakika za mwisho kwenda kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa michezo.
Hiyo inakuwa kazi ya kwanza kwa Mourinho ambayo haitahusiana na ukocha na siku za karibuni, amehusishwa pia na Chelsea baada ya kuondoka Kocha Mauricio Pochettino.
Awali alihusishwa na Liverpool baada ya Jurgen Klopp kuondoka, lakini miamba hiyo ya Anfield imeshapata kocha mpya, Mdachi Arne Slot.
Hata hivyo, Mourinho ameweka wazi hakubali tu kwenda kujiunga na timu kwa sababu anataka kazi, bali anazingatia mipango ya timu hiyo kwenye kunasa mataji na kuwa na vikosi bora.