Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Motsepe kwa bao la Aziz Ki amejaribu kuchutama vyema

Patrice Motsepe 2 1062x598 Rais wa shirikisho la soka Barani Afrika Patrice Motsepe

Mon, 27 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Patrice Motsepe. Mtu na pesa zake. Ana utajiri wa Dola 3 bilioni. Haupati ubilionea kama hauna akili. Sio lazima ziwe akili za darasani. Zinaweza kuwa za namna nyingine. Nilimfurahia Motsepe na akili zake aliposimama mbele ya vipaza sauti vya waandishi wa habari katika ardhi ya Mama Kizimkazi pale Zanzibar Ijumaa asubuhi.

Alijua Watanzania wanataka kusikia nini kutoka kwake na akawapa ambacho walikuwa wanataka kusikia. Wakati mwingine unaamua kuufunga mjadala kiufundi zaidi. Sidhani kama alishinikizwa alichosema. Sijui kama aliulizwa swali akalazimishwa kujibu. Hapana. Alijua yupo na jibu sahihi katika ardhi sahihi na zaidi ya kila kitu ni katika wakati sahihi.

Kwamba anadhani bao ambalo Stephane Aziz Ki alifunga dhidi ya timu yake Mamelodi Sundowns pale Pretoria lilikuwa bao halali. Ni kwamba anaacha tu mamlaka za waamuzi zifanye kazi yake. Motsepe alijaribu kutumia akili ambayo watu wachache tulikuwa mbele yake, lakini akakusanya watu wengi ambao labda wanashindwa kufikiria kwa haraka maisha ya nyuma ya pazia. Unahitaji jicho la mwewe kumuelewa.

New Content Item (1)

Kwanza kabisa huu ni ugumu wa kuwa Rais wa CAF, halafu hapo hapo una timu kubwa barani Afrika ambayo unaimiliki. Kule Uingereza, kabla ya Ligi Kuu ya England kuanza waamuzi wote huwa wanaitwa na kuulizwa timu ambazo wanashabikia. Kama unavyofahamu wazungu wengi wanashabikia timu za vitongoji vyao. Ni wachache ndio ambao wanaonekana wanashabikia timu kubwa.

Kama ikitokea unashabikia timu ya Ligi Kuu huwa haupangwi katika mechi zake. Lakini pia huwa haupangwi katika mechi ambazo kwa namna fulani zinaweza kuiathiri timu yako. Wenzetu wametumia akili hii kwa makusudi kabisa wakizingatia ubinadamu wa mwanadamu.

Motsepe amejikuta akiwa ni Rais wa CAF na mmiliki wa Mamelodi Sundowns. Inawezekana hana upendeleo wa moja kwa moja, lakini waamuzi pia ni binadamu. Wanamjua bosi wao ni nani. Maamuzi yoyote ambayo yanaonekana kuipendelea Mamelodi moja kwa moja huwa yanahusishwa naye. Iwe kwa yeye kuonekana amefanya mipango au kwa waamuzi kumuogopa.

Kule Ivory Coast rafiki zetu wa Afrika Kaskazini walilalamika kwamba uwepo wa Motsepe katika mechi za Afrika Kusini ulikuwa unawatisha waamuzi, hivyo walikuwa wanalazimika kufanya maamuzi ya kuwapendelea kila wakati. Siamini kama ilikuwa kweli, lakini ukiwa Rais wa CAF halafu timu yako ipo katika michuano basi hata hadithi hii ukimsimulia mtoto mdogo anaweza kuiamini.

Na sasa Motsepe alikuwa amesimama mbele ya vipaza sauti pale Zanzibar akijaribu ‘kuoga’. Alidai kwamba anaamini kuwa bao la Aziz Ki lilikuwa sahihi. Ni kweli lilikuwa sahihi. Wote tumeona. Kujikosha kwake kulikuwa kunamaanisha kwamba alikuwa anawaonea huruma Yanga na kwamba hakuhusika kwa lolote katika tukio lile. Na kwamba pia huwa hausiki kwa lolote katika kutoa mashinikizo kwa waamuzi.

Ni suala la kumuua mtu usiku wa manane na usionekane. Kesho yake unaamkia katika msiba wa mtu huyo huyo na kuanza kulia kwa nguvu. Ni rahisi kwa watu kutokukuhisi. Imetokea hivyo mara nyingi katika maisha ya wanadamu na huwa inahitaji uchunguzi mkubwa kukamilisha upelelezi.

Haya anayafanya pia wakati huu akiwa ni rafiki mkubwa wa Watanzania. Motsepe ni rafiki wa Wallace Karia. Ni rafiki wa Wilfred Kidao. Zaidi ni rafiki wa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said. Anawapenda Watanzania na ndio maana aliwapa pia nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano ya Shule za Afrika (ASFC 2024) pale Zanzibar.

Lakini alitupa uenyeji wa michuano ya African Football League ambayo Simba ilicheza pambano la kwanza la ufunguzi dhidi ya Al Ahly pale Temeke. Hapo hapo anajua kwamba Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zina kura yake katika nafasi anayokalia. Kwanini uweke mazingira ya chuki? Hakukuwa na haja.

Alichoongea kuhusu bao la Aziz Ki ni kweli, lakini alitumia fursa hiyo kuwapoza Watanzania. Chochote ambacho angesema tofauti kuhusu lile bao angeongeza chuki zilizo katika vifua vya Watanzania dhidi yake. Akaamua kuucheza mchezo salama ambao kwa sasa unaruhusiwa kwa sababu na Mamelodi wametolewa.

Kama Mamelodi wangekuwa bado katika michuano halafu Motsepe akasema anachosema ina maana kwamba watu wangetafsiri kwamba kama wakichukua ubingwa basi utakuwa haramu. Motsepe alikuwa huru kusema alichokisema kwa sababu Mamelodi wametolewa katika michuano. Matajiri hawapati utajiri kwa bahati mbaya. Wana akili.

Ninachomuonea huruma Motsepe katika nafasi aliyonayo ni ukweli atakazimika kuishi katika mazingira haya magumu kwa muda mrefu ambao ataendelea kukaa madarakani. Zaidi ni kwamba Mamelodi wapo katika vita na timu za Afrika Kaskazini. Wao ndio watu wa ukanda mwingine ambao wanaonekana kuwa tishio zaidi kwao.

Mfano mwingine ni namna ambavyo Afrika Kusini ina nafasi ya kuandaa michuano mingi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla kutokana na mazingira ya uchumi wao na ubora wa nchi yao. Hata hivyo, leo hii Afrika Kusini wakiandaa michuano yoyote ile itaonekana ni kwamba Rais wao amejipendelea. Watu watasahau kuwa, Afrika Kusini ilishaandaa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 huku Motsepe akiwa sio Rais.

Lakini watu hawatasahau pia pesa zake. Watasema kwamba anatumia cheo na utajiri wake kuinufaisha Afrika Kusini. Nongwa hizi zitaendeshwa zaidi na watu wa Afrika Kaskazini ambao kwa muda mrefu wameishika CAF mkononi. Hawa ndio walisababisha makao makuu ya CAF yawe Misri. Ukweli ni kwamba wanajua mpira lakini wanajua fitina za mpira pia katika kiwango cha juu. Kwa sasa hawana raha na Urais wa Motsepe

Bao la Aziz Ki lilikuwa katika vipaumbele vya habari kule Afrika Kaskazini kama ilivyokuwa kwa Tanzania. Waarabu walijua kuna fitina imefanyika. Lakini sio kwamba wanatupenda, hapana, walipenda zaidi Yanga isonge mbele kwa sababu kwao kungekuwa na urahisi mkubwa wa kuitoa mbele ya safari kuliko kuitoa Mamelodi.

Usisahau pia nongwa hizi zitaendeshwa pia na Waafrika wanaotoka nchi zinazoongea Kifaransa ambao kwa muda mrefu wameishika CAF kuliko wale wanaotoka katika nchi zinazoongea Kiingereza. Afrika ina mapande haya mawili ambayo yana siasa zake kwa kiasi kikubwa. Upande mwingine Motsepe ni mtu sahihi kwetu kwa siasa za kikoloni.

Jambo la msingi ambalo litamuweka Motsepe salama zaidi ni kupambana na kuhakikisha soka la Afrika linaendeshwa kwa haki. Miongoni mwa akili hizo ni kutumia kwa haki zaidi matumizi ya teknolojia. Bao la Aziz Ki halikuhitaji VAR. Lilihitaji Goal Line Technology. Basi. Katika VAR wanaweza kukaa wahuni kama wahuni wengine tu.

Wazungu ni watu walioonyoka na waliamua kuunyoosha mpira wao. Hata hivyo, ndani ya VAR zao bado kuna watu wachache wameamua kuendeleza uhuni wao na ndio maana majuzi klabu ya Wolves iliamua kupeleka muswada wa kutaka VAR ifutwe. Sijui itaamuliwaje, lakini naamini wazungu hawawezi kutaka turudi tulikotoka. Soka lipo kwa Motsepe sasa hivi.

Chanzo: Mwanaspoti