Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Motsepe kufuta Kombe la Shirikisho Afrika mjadala mzito

Patrice Motsepe AFL.jpeg Motsepe kufuta Kombe la Shirikisho Afrika mjadala mzito

Wed, 17 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ishu ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kutazamiwa kuyafuta mashindano yake ya pili kwa ukubwa ya Kombe la Shirikisho, kulingana na ripoti zilizopo, inaonekana kuzua mijadala kwa sasa katika mitandao ya kijamii.

Kombe la Shirikisho Afrika ambalo lilianzishwa 2004 kutokana na kuunganishwa kwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi muda wowote linaweza kutangazwa kufutwa kama alivyosema rais wa CAF, Patrice Motsepe mwanzoni mwa mwaka huu kule Ivory Coast wakati wa fainali za mataifa ya Afrika.

Motsepe alisema, "Tunaweza kufuta Kombe la Shirikisho. Tuna mashindano mengi sana. Hatuwezi na hatutakuwa na mashindano mengi ....Ligi ya Mabingwa ni bora; tunataka kuilinda na kuikuza. Ndio maana sikuweka kwa makusudi pesa za AFL kuwa zaidi ya Ligi ya Mabingwa. Sikutaka kujenga dhana kwamba, AFL iko juu ya Ligi ya Mabingwa."

Kauli hiyo kwa sasa inatafsiriwa kwamba mchakato huo umeiva hivyo klabu za Tanzania, Simba, Yanga, Azam na nyinginezo ambazo zinapigania nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao wanatakiwa kuwa tayari na hili.

Kufutwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika kuna maana kuwa michuano ya kimataifa katika ngazi ya klabu itasalia miwili, Ligi ya Mabingwa Afrika na AFL.

Itakuwaje sasa? Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itachukua nafasi ya Kombe la Shirikisho la CAF kama shindano la pili la klabu barani Afrika.

Mshindi wa African Footabll League sasa ataliwakilisha bara katika Kombe la Dunia la klabu la FIFA.

Mchakato utakuwaje? Mara ya baada ya CAF kutangaza rasmi kufutwa kwa Kombe la Shirikisho basi watatoa muongozo wa namna mambo yatakavyokuwa. Lakini pamoja na hayo, Tanzania ni kati ya nchi ambazo zinaweza kuendelea kutoa klabu nne kwa ajili ya michuano hiyo ya kimataifa.

Bingwa wa Ligi na mshindi wa pili walikuwa wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku anayeshika nafasi ya tatu na bingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) hushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbukwe kuwa washiriki wa kombe la African Footaball League ambalo uzinduzi wake ulifanyika Tanzania kwa mchezo kati ya Simba na Al Ahly huteuliwa tu kulingana na kufanya kwao vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kati ya maswali ambayo wadau wengi hujiuliza ni je, itakuwaje kwa wale ambao walikuwa wakishiriki michuano ya kimataifa kwa njia ya Kombe la Shirikisho baada ya michuano hiyo kufutwa?

Baada ya Simba na timu nyinginezo kutolewa, Kombe la Shirikisho limeingia hatua ya robo fainali ambapo droo yake imefanyika leo kwa mabingwa watetezi Yanga kupangwa dhidi ya Tabora United, Azam itaikabili Namungo, Ihefu itaivaa Mashujaa, wakati Coastal Union itacheza na Geita Gold FC.

Kufutwa kwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kunahofiwa kutaleta tafsiri kwamba michuano hii ya Shirikisho Tanzania, ambayo imefika hatua ya robo fainali itapoteza maana yake ya awali na kubaki kuwa kama bonanza tu, au inaweza kuchukua sura mpya ya michuano mingine ya ndani ambayo mshindi wake hueshia kutwaa kombe na zawadi mbalimbali zikiwamo za fedha na haendi kucheza michuano ya ngazi ya bara (continent) kama ilivyo michuano ya Kombe la Ligi (maarufu EFL au Carabao) kwa England.

Chanzo: Mwanaspoti