Imebakia miezi sita kabla ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kufanya uchaguzi mkuu wa kuchagua viongozi wake kwa awamu inayofuata kuanzia 2025 hadi 2029.
Kama utaratibu utaenda kama inavyohitajika na matakwa ya katiba ya CAF, uchaguzi huo utafanyika Machi mwakani katika nchi ambayo itapangwa kuandaa mkutano mkuu wa shirikisho hilo ambao miongoni mwa agenda zake ni uchaguzi.
Nafasi ambazo zitagombewa kikatiba ni ya Urais, 13 za ujumbe wa kamati ya utendaji ambazo kati ya hizo, moja angalau inatakiwa iende kwa mwanamke na nafasi sita za kuiwakilisha Afrika katika baraza la Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FiFA).
Ikumbukwe kwa mujibu wa katiba ya CAF, uchaguzi wa Rais na wajumbe wa kamati ya utendaji unafanyika kila baada ya kipindi cha miaka minne hivyo ifikapo Machi mwakani ndio itakuwa ukomo wa awamu ya sasa ya uongozi chini ya Rais Dk. Patrice Motsepe kutoka Afrika Kusini.
Ikiwa imebakia miezi sita kabla ya uchaguzi huo, hadi sasa Motsepe bado hajatangaza au kuonyesha nia hadharani kuwa atagombea kuomba ridhaa ya kuiongoza CAF kwa awamu ya pili baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza iliyoanza 2021 alipoingia madarakani.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwa Motsepe kuingia katika kinyang’anyiro cha kutetea tena nafasi yake kwa vile amekuwa akipigiwa chapuo na viongozi wa vyama vingi vya soka Barani Afrika aendelee kuongoza chombo hicho chenye mamlaka ya kusimamia mpira wa Afrika.
Kuna sababu kadhaa ambazo zinashawishi idadi kubwa ya viongozi wa vyama vya mpira wa miguu Afrika kutamani Motsepe aendelee kuiongoza CAF na hivyo kumuweka mmiliki huyo wa zamani wa klabu ya Mamelodi Sundowns katika uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa katika wadhifa huo wa Urais kwa awamu nyingine.
Sababu ya kwanza ambayo inambeba Motsepe ni namna uongozi wake ulivyoonyesha msisitizo na mkazo katika kusimamia suala la miundombinu ya soka tangu alipoingia kwa madarakani hadi leo hii.
Uongozi wa Motsepe umeonekana kuweka kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha viwanja vya soka vinavyotumika kwenye mashindano mbalimbali barani humu vinakuwa na ubora wa hali ya juu tofauti na ilivyokuwa zamani.
Tumeona viwanja vingi ambavyo havina ubora vikizuiwa kutumika kwa mechi zilizo chini ya CAF na hata Fifa jambo ambalo linalazimisha nchi ambazo viwanja husika vipo, kuviboresha ili vipewe hadhi ya kuandaa mechi kubwa.
Na iko wazi kwamba ubora wa viwanja una mchango mkubwa katika kukuza soka katika nchi husika na kuimarisha viwango vya wachezaji.
Kingine ambacho uongozi wa Motsepe umefanikiwa ni kuchukua hatua kadhaa za kuziimarisha timu kiuchumi kuanzia zile za klabu hadi za taifa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likisaidia kuongeza ushindani katika soka la Afrika.
Mfano hivi sasa, CAF inatoa kiasi cha Dola 50,000 (Sh136 milioni) kwa timu zote ambazo zinashiriki mashindano ya klabu Afrika, fedha ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuziwezesha timu kumudu gharama za ushiriki kwenye mashindano hayo.
Kwa timu za taifa tumeshuhudia CAF ikitoa kiasi cha Dola 500,000 (Sh1.4 bilioni) kwa timu zote ambazo zinaishia katika hatua ya makundi ya fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) hii ikimanisha kwamba kitendo tu cha timu kufuzu fainali hizo, inajihakikishia kiasi hicho cha fedha.
Tumeona Motsepe pia akiamua kutoa uwezeshaji wa kifedha kwa wenyeviti na marais wa vyama na mashirikisho ya soka kwa nchi wanachama wa CAF ambapo kila mmoja atapata kiasi cha Dola 50,000 kwa mwaka.
Sababu nyingine ni kuboresha mfumo wa mashindano ya klabu Afrika katika namna kadhaa mojawapo ikiwa ni kuondoa kanuni ya kuziruhusu timu zinazotolewa kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuangukia katika hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa sasa, timu zilizopo katika Kombe la Shirikisho Afrika, zinacheza raundi mbili tu kabla ya hatua ya makundi tofauti na zamani ambapo zilikuwa zinacheza raundi tatu.
Hii inasaidia kuongeza ushindani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kupandisha thamani ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ameongeza wigo wa mashindano kwa kuanzisha mashindano ya African Football League ambayo tayari yameshachezwa mara moja.
Eneo lingine ambalo Motsepe amefanikiwa ni kuimarisha kiwango cha uchezeshaji kwa marefa na usimamizi mzuri wa mashindano.
Hii imesaidia kupatikana kwa matokeo ya haki na kupunguza hujuma kwa timu mbalimbali tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita kabla yake.
Katika maisha, hakuna mwanadamu ambaye amekamilika hivyo hata Motsepe na uongozi wake kuna baadhi ya mambo hawaja sahihi lakini ukiweka katika mzani utaona yale ambayo amepatia ni mengi kuliko yale ambayo amekosea.
Kiongozi kama huyu ambaye ameonyesha nia ya kuendeleza mpira wa Afrika kwa vitendo, anapaswa kupata sapoti na uungwaji mkono ili yale aliyoyaanzisha aweze kuyaendeleza.
Kwa mtazamo wangu, Motsepe anastahili kuendelea kupewa dhamana ya Urais wa CAF pindi muda wa uchaguzi wa shirikisho huo utakapofika mwakani.