Moja ya maeneo muhimu sana kwenye mchezo wa soka ni eneo la kiungo. hapo ndipo mipango yote inasukwa, kiufupi ni kama 'injini' ya timu kwani ni eneo ambalo wachezaji wake wanatakiwa kuhusika kikamilifu wakati wote timu inapokuwa na mpira na ambapo haina mpira.
Safu ya kiungo inahusika kwenye kuanzisha na kutengeneza mashambulizi lakini pia kulinda na kuzuia mashambulizi baina yao hivyo kulifanya kuwa miongoni mwa maeneo spesho zaidi uwanjani.
Katika miaka ya hivi karibuni soka linachezwa kwa mifumo na sayansi zaidi na hapo ndipo thamani ya viungo inazidi kupanda kutokana na mahitaji na faida zao katika timu.
Hilo limepelekea mechi nyingi kwa sasa kuamuliwa na eneo la kiungo ambapo kama timu A itakuwa na viungo bora kulio timu B, basi inaweza kushinda na kumaliza mechi kwa aina watakayo na huenda ndio maana viungo wengi siku hizi 'wanajisikia' (Utani).
Jumapili ya April 16 pale uwanja wa Benjamin Mkapa kutakuwa na mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga ikitarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake lakini katika jicho la kiufundi huenda viungo wa timu zote mbili wakaamua mechi hiyo inayosubiliwa kwa hamu na mashabiki wa soka Afrika na Dunia kwa ujumla.
Simba na Yanga zote uimara wake kwenye viungo sio jambo la kutilia shaka na kila timu ina machaguo zaidi ya mawili katika kila kipande katika eneo la kiungo na vipande hivyo ni viungo wakabaji na viungo washambuliaji.
Kwa Simba ambao ni wenyeji eneo lao la kiungo wazuiaji huwa wanacheza, Sadio Kanoute, Jonas Mkude, Ismael Sawadogo, Nassoro Kapama, na Erasto Nyoni huku viungo washambuliaji wakiwa Mzamiru Yassin, Clatous Chama na Said Ntibazonkiza 'Saido'.
Upande wa Yanga eneo la viungo wazuiaji wamekuwa wakicheza Yanick Bangala, Zawadi Mauya, Kharid Aucho na Mudathiri Yahya anayecheza pia eneo la kiungo mshambuliaji sambamba na Salum Abubakar 'Sure Boy', Stephane Aziz Ki na Farid Mussa.
Hata hivyo kutokana na namna timu hizo mbili zimekuwa zikicheza kwenye vikosi vyao vya hivi karibuni kuna baadhi ya wachezaji katika eneo la kiungo wananafasi kubwa ya kuanza katika vikosi vya kwanza mechi ya jumapili na huu hapa ni uchambuzi wa namna wanaweza kuzisaidia au kuziponza timu hizo.
KANOUTE V AZIZI KI
Simba imekuwa ikimtumia mara kwa mara Kanoute kama kiungo wa chini (namba sita), kwa maana hiyo jukumu lake ni kumkaba kiungo wa juu wa timu pinzani (namba 10), na kwa Yanga nafasi hiyo amekuwa akicheza Aziz Ki hivyo hapa kutakuwa na bato la aina yake kama ataanza wawili hawa.
Aziz Ki ana ubora wa kupiga pasi, chenga kukimbia na kufunga huku Kanoute akisifika kwa kukaba kwa nguvu, kuziba nafasi na kupiga pasi jambo ambalo linaweza kuleta ushindani katika eneo hilo hadi sasa.
Hadi sasa kwenye ligi Aziz Ki ana mabao nane na asisti idadi nzuri kwa kiungo mshambuliaji huku Kanoute akiwa na sifa yaq kuzuia kwa maarifa licha ya kucheza faulo mara kwa mara ambazo pia Aziz Ki ni mtaalamu wa kuzitumia.
MZAMIRU V MUDATHIR
Hapa ni vita ya kweli kati ya viungo hawa wawili ambao mara nyingi hutumiwa kama viungo wa kati, hapa huwa katikati ya uzuiaji na ushambuliaji.
Kasi, chenga na ubora wa kupiga pasi kwa wachezaji wote wawili vipo na ubora wao haupishani sana kutokana na wanavyocheza lakini kama ilivyo mpira wa miguu ni mchezo wa makosa basi atakayefanya kosa kati ya hawa huenda akamnufaisha wengine. Hadi sasa Mzamiru ana mabao mawili na asisti tano kwenye Ligi huku Mudathiri aliyeingia Yanga katika dirisha dogo namba zake kwa ujumla kwenye ligi zikiwa chini ya tano. mawili,
CHAMA V AUCHO
Vita nyingine tamu kutizama ni kati ya Chama na Aucho, wawili hao wote wana uzoefu wa kutosha na mechi za aina hii, na wanajuana vyema jambo linaloongeza radha ya dabi.
Chama ni bora zaidi kwenye kutengeneza nafasi za mabao na kufunga akiwa kinara wa asisiti (14) hadi sasa kwenye ligi sifa ambayo pia anayo Aucho. ukiachana na uzoefu wa wakali hawa jambo lingine linaloweza kuleta maafa kwa upande mmoja ni maamuzi na kujiamini kwao wanapokuwa na mpira.
SAIDO V BANGALA
Hapa pia kuna bato ya aina yake, Saido mwenye mabao 10 na asisti nane hadi sasa kwenye ligi atakutana na Bangala mwenye asili ya beki na bora katika umiliki mpira na kupiga pasi.
Kila mchezaji ana uzoefu wa kutosha na mechi kubwa na wote wana kariba ya hasira na sifa hivyo ni miongoni mwa maeneo yatakuwa na udambwi wa hali ya juu kama watapangwa wote.
WASIKIE WATAALAMU
Kiungo wa zamani Simba na Yanga Athumani Iddi 'Chuji' alisema licha kuwepo kwa wachezaji bora katika maeneo tofauti, viungo ni baadhi ya wachezaji wanatakiwa kuwa bora kwenye mechi hiyo ili kuzisaidia timu zao.
"Kiungo ndio muhimili wa timu, hata kama timu ina wachezaji bora katika maeneo ya mengine lakini viungo wakiyumba ni rahisi zaidi kwa timu kupoteza balansi," alisema Chuji na kuongeza;
"Simba na Yanga zote zina viungo bora kwa sasa na kila upande unaweza kuwawini wenzake na mara nyingi mechi hizi hazitabiriki hivyo watakaoamka vizuri ndio watazisadia timu zao."
Mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mrisho Ngassa ambaye pia aliwahi kuzichezea Simba na Yanga kwa mafanikio alisema kila mchezaji ndani ya timu ana umuhimu wake lakini kwa namna mpira wa sasa ulivyo viungo ni miongoni mwa watu wanaoweza kuamua mechi.
"Zamani mara nyingi wafungaji walikuwa washambuliaji, sikuhizi mambo yamebadilika na kila mtu anafunga hivyo hata viungo wanaweza kuamua mechi na katika dabi natarajia kuona ubora wa aina yake eneo hilo kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili," alisema Ngassa anayeendesha kituo chake cha kukuza vipaji kinachoitwa Enjoy Soccer Academy kilichopo Boko Dar es Salaam.