Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba, Boniface Lihamwike, ametangaza majina 14, yaliyopitishwa na kuruhusiwa kuanza rasmi kampeni kuanzia jana hadi Januari 28 kuelekea uchanguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari 29, mwaka huu.
Wagombea waliopita katika nafasi ya Mwenyekiti ni wawili, ambao ni wakili Mosses Kiluwa na Murtaza Mangungu anayetetea nafasi yake ya uenyekiti baada ya kumaliza muda wake.
Wajumbe ni Seif Muba, Seleman Haroub, Idd Kitete, Issa Masoud, Abubakari Zebo, Abdallah Mgomba, Edward Mweladzi, Rashid Khamsini, Asha Baraka, Pendo Aidan, Rodney Karambo na Aziz Mohamed.
Akizungumza na gazeti hili jana, Lihamwike alisema baada ya kupitisha majina hayo wagombea wanatakiwa kuanza rasmi kampeni ambazo zitadumu hadi Januari 28 kabla ya uchaguzi huo kufanyika Januari 29, mwaka huu.
Aliwataka wagombea hao kufanya kampeni kwa kuzingatia katiba ya nchini na kanuni zinazowaongoza kwa sababu lengo ni kuona uchaguzi ukiwa wa haki na wazi ili kupata viongozi walio sahihi.
“Mchakato wa uchaguzi ulianza Novemba 26, mwaka jana kwa kupitia majina mbalimbali ikiwamo kufanya tathmini, pingamizi na wale waliokata rufaa katika Kamati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kujiridhisha, tunatamka majina hayo 14 rasmi wataanza kampeni za uchaguzi,” alisema Mwenyekiti huyo.