Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Morrison mtu mbaya, 300M za GSM zabebwa kwa jasho na damu

98539 Morrison+pic Morrison mtu mbaya, 300M za GSM zabebwa kwa jasho na damu

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

YANGA wabayaa haoo...Morrison Mutu Mubaya huyo...BM3 Mutu Mubaya....Hilo ni songi lililongurumishwa na mashabiki wa Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, wakiwa na furaha ya chama lao kuwanyoosha Simba kwa bao tamu la ‘frii-kiki’ ya moja kwa moja lililowekwa kimiani na Bernard Morrison a.k.a MB33.

Morrison aliyekuwa akicheza derby yake ya kwanza, kama ilivyokuwa kwa kipa Metacha Mnata, alifunga bao hilo dakika chache kabla ya mapumziko na kuipa ushindi wa kwanza timu yake tangu mwaka 2016 na kufuta uteja wa misimu mitatu mfululizo.

Yanga ilishinda mara ya mwisho Februari 20, 2016 walipoitungua Simba kwa mabao 2-0 na kuishia kuambulia vipigo vitatu na sare nne na kwenye pambano la jana lililoshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, mashabiki wengi wa Simba walijiamini timu yao ingeendeleza ubabe.


Mbali na Morrison, kipa Metacha Mnata ndiye aliyeonekana kuwa nyota wa mchezo kwa namna alivyokuwa akiokoa michomo ya wazi ya Simba ambao ilitawala kwa sehemu kubwa ya mchezo.

Pia Soma

Advertisement

Kabla ya mchezo huo Kocha wa Yanga, Luc Aymael alienda kuugusa mpira ukiwa kwenye kifaa chake na kisha kuonyesha alama ya msalaba, ishara iliyotafsiriwa na mashabiki wa Yanga kama aliubariki mpira huo uliotumbukizwa kimiani na winga wake kutoka Ghana.

WAAMUZI SITA, BURUDANI

Kwa mara ya kwanza, mchezo huo ulichezeshwa na waamuzi sita. Kati alikuwapo Martine Saanya, akisaidiwa na Mohammed Mkongo, Frank Komba pembeni na nyuma ya magoli walikaa Abdallah na Ramadhani Kayoko na Elly Sasi alikuwa wa akiba.

Hata hivyo, wingi huo wa waamuzi haukufanya pasiwepo na malalamiko ya uamuzi, kama wachezaji wa Yanga walipotaka Clatous Chama aonyeshwe kadi nyekundu kwa kumkanyaga kwa makusudi kwenye kiazi cha mguu Feisal Salum aliyekuwa ameanguka chini.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Mbali na kupata bao la kuongoza dakika ya 44, likifungwa na Morrison, kipindi cha kwanza kilikuwa cha matukio mchanganyiko, Yanga wakitawala eneo la kiungo huku Simba wakiwa tisho zaidi katika eneo la ushambuliaji.

Metacha akaokoa

Yanga ilifanya shambulio katika dakika ya 10 kupitia kwa Ditram Nchimbi shuti lilitoka nje, pia dakika ya 11 likatoka mita moja kutoka golini.

Kocha wa Simba, Sven alifanya mabadiliko kwa kumtoa Erasto Nyoni akaingia Kennedy Juma dakika ya 22 kutokana na kiraka huyo kupata maumivu ya mguu kama ilivyokuwa kwa Morrison kipindi cha pili aliyempisha Patrick Sibomana.

Simba itajilaumu kwa kushindwa kuibuka na ushindi kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi kwa mashuti yaliyolegwa na nyota wake wakiongozwa na Luis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco, Francis Kahata na baadaye Deo Kanda.

Katika kipindi cha pili Eymael mbali na kumpumzisha Morrison dakika 50, pia alimtoa Mapinduzi Balama na kumuingiza Deus Kaseke na Feisal Salum akampisha Kelvin Yondani, huku Sven Vanderbroeck wa Simba, akimtoa Kahata na kumuingiza Kanda na wakati Kagere alimpisha Hassan Dilunga na kuongeza utamu wa mchezo huo, Simba ikisaka bao la kusawazisha na Yanga ikitaka kuongeza.

Dakika za majeruhi, Kaseke alishindwa kukwamisha mpira kimiani kwa kupiga shuti lililogonga nguzo na kuokolewa na mabeki, huku Deo Kanda naye akipoteza nafasi ya wazi ya kusawazisha katika dakika hizo na mpaka kipyenga cha mwamuzi, Martin Saanya kikilia, Yanga walikuwa wababe.

Magufuli naye ndani

RAIS wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli aliwasapraizi mashabiki kwa kutinga uwanjani robo sasa kabla ya kuanza kwa pambano hilo lililochezwa kuanzia saa 11 jioni, akiwa ametinga uzi wenye mseto wa jezi ya Yanga na Simba akifuatana na msafara wa Rais wa CAF, Ahmad Ahmad.

Mara alipotinga JPM alisalimiana na viongozi wa TFF na kuelekezwa sehemu ya kukaa kabla ya kulishangilia bao la BM33 kwa kupunga mkono hewani.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kuishuhudia Simba ‘ikitobolewa tobo’ akiwa kwenye Uwanja wa Taifa, mara ya kwanza ikiwa Mei 10 mwaka jana wakati Simba ikilala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Simba, Yanga dakika 21 tu

Kwenye mchezo huo wa jana, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kuingiza uwanjani, wakiitangulia

Msafara wa vinara hao wa Ligi Kuu, uliokuwa na magari manne na kusindikizwa na pikipiki ulitinga Taifa, saa 9:06 alasiri na kupokelewa kwa shangwe na mashabiki wa timu hiyo.

Baada ya kuingia Taifa, mashabiki wa Simba waliizingira basi ya wachezaji na baadhi yao kuifuata nyuma huku wakishangilia kama kuwapa mzuka nyota wao.

Ndipo ilipotimu saa 9:27 alasiri, msafara wa Yanga waliokuwa wenyeji wa mchezo waliwasili Taifa wakiwa na magari matatu na kusindikizwa na eskoti ya pikipiki mbili na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wao na kuuchuna mpaka saa 9:32 waliposhuka wachezaji, wakiongozwa na Juma Abdul.

Yanga walipishana dakika nane tu na waamuzi waliotanguliza kuwasili uwanjani saa 9:30 alasiri wakiwa kwenye gari moja.

Makomandoo wazichapa

Mara baada ya Yanga kuwasili uwanja, mashabiki wa klabu hiyo waliamua kuchapana makonde, baada ya mmoja wao kuzingua wakati akilazimisha kuingia kwenye vyumba vya wachezaji.

Ishu ilikuwa hivi. Baada basi la wachezaji kuegeshwa eneo lililotengwa, nyota wa Yanga walianza kushuka na kuingia vyumbani, ambao mlangoni kulikuwa na baadhi ya askari Polisi, walinzi na makomandoo wa timu hiyo waliokuwa wakihakikisha usalama, wengine wakilinda yumba vyao na kuzuia hujuma zote.

Ghafla akatokea komandoo mmoja, aliyekuwa akitaka kueleka vyumbani ndipo sekeseke lilipoanza baada ya wenzake kumzuia kwa kuambiwa haruhusiwi yeyote kuingia vyumbani zaidi ya wachezaji na watu maalum waliopangwa na kusababisha makomandoo hao kushika mashati.

Tafrani hiyo ilidumu kwa dakika mbili kabla ya askari Polisi na baadhi ya viongozi wa Yanga akiwemo Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz kuwaamulia aliyetaka jamaa aruhusiwe kwenda ndani kwani anafahamika.

Tukio lingine lililotokea wakati timu ikiingia ni makomandoo hao kuwazuia waandishi wa habari kuchukua picha na video kwa madai wanatumika na wapinzani wao Simba.

Vikosi vilivyoanza;

YANGA: Metacha, Abdul, Jafar, Lamine, Makapu, Tshishimbi, Balama, Fei Toto, Nchimbi, Niyonzima na Morrison

SIMBA: Manula, Kapombe, Tshabalala, Nyoni/Kennedy, Wawa, Mkude, Miquissone, Chama, Kagere, Bocco na Kahata.

Chanzo: mwananchi.co.tz