KAMATI ya Sheria ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewapiga faini ya jumla ya Sh milioni 15, Ofi sa Habari wa Simba, Haji Manara, Ofi sa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Zacharia Hanspoppe, kwa kukutwa na makosa ya kinidhamu.
Manara, Hanspoppe na Bumbuli, wote makosa yao yametokana na sakata la mchezaji Benard Morrison, ambaye Agosti, mwaka huu alikuwa na mvutano kati yake na timu aliyokuwa akiichezea msimu uliopita, Yanga.
Mbali na faini hizo, kamati hiyo pia imewataka kujichunga na kutofanya makosa ya kinidhamu kwa kipindi cha miaka miwili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Kichere Mwita, alisema watatu hao wamekutwa na hatia baada ya kumati hiyo kujadili makosa yao.
Alisema kwanza walianza kusikiliza shauri la Manara, ambaye Agosti 11, mwaka huu alizungumza kwenye chombo cha habari maneno ya kutuhumu na kutishia kuingilia Kamati ya Katiba na Sheria ya TFF katika kipindi ambacho ilikuwa ikiendelea kusikiliza shauri la Yanga na Morrison.
Alisema pia kamati hiyo imemtia hatiani Bumbuli kwa kosa la kutoa taarifa za uongo, akieleza umma kupitia chombo cha habari kuwa hakupata nakala ya hukumu ya kesi ya Morrison, jambo ambalo halikuwa kweli kwani Yanga walishaipata siku moja iliyopita.
Kwa upande wa Hanspoppe, Kichere alisema kuwa, akiwa mjumbe wa Kamati ya Katiba alisikika kwenye chombo cha habari akieleza maamuzi ya kesi ya Morrison bila ya kuwa na ruhusa ya mwenyekiti.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema licha ya kukutwa na hatia hiyo, wanaruhusiwa kukata rufaa kama hawatoridhishwa na maamuzi hayo.
“Kamati imempiga faini ya Sh milioni 5 na kumtaka kutofanya kosa la kinidhamu ndani ya kipindi cha miaka miwili, Haji Manara, kwa kosa la kutoa kauli za kutuhumu na kutishia kuingilia maamuzi ya Kamati ya Katiba akiwa ni msemaji wa Simba,” alisema.