Straika wa zamani wa Orlando Pirates, Bernard Morrison amewaambia Kaizer Chiefs kwanini Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ni chaguo sahihi kwao kwa sasa.
Morrison ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Yanga, amewaambia Kaizer kwamba miaka miwili ya Nasreddine Nabi Jangwani amejifunza mengi na ameiva kuchukua nafasi ya Arthur Zwane anayetajwa kulipwa Sh100milioni kwa mwezi.
Morrison alinukuliwa na Gazeti la FARPost la Afrika Kusini jana kwamba; "Anajua kwamba kwenye hizi klabu kubwa,ukipoteza moja na sare moja umeondoka. Kwahiyo anajua presha iliyopo."
“Amekuwa hapa Yanga kwa karibu miaka miwili, nadhani kwenda kwenye klabu kubwa kama za Afrika Kusini anajua jinsi ya kudili na presha. Anajua kwamba lazima apate matokeo mazuri, kama hatayapata watamtimua.
"Kwahiyo lazima awe tayari kwa hali yoyote,"alisema Morrison ambaye anahusishwa na klabu ya Singida United msimu ujao.
Habari za uhakika ni kwamba Nabi jana alikuwa kwenye mazungumzo na Kaizer na amewaambia mambo kadhaa anayotaka ikiwemo timu yake ya ufundi na yeye inaelezwa atalipwa donge nono la Sh100milioni anazolipwa Kocha wa sasa ambaye wanataka kumtoa baada ya kushindwa kutimiza malengo.
Nabi amewaambia anataka kwenda na Kocha Msaidizi, Kocha wa Makipa pamoja na mtu wa video na inaripotiwa siku yoyote wiki hii atatua Sauzi kumaliza dili.
PRESHA KUBWA
Tajiri wa Yanga Ghalib Said Mohamed 'GSM' ameanza hesabu mpya kuanzia leo kuhakikisha anambakiza Nabi na kundi la wasaidizi wake.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ambazo Mwanaspoti halina shaka nazo ni kwamba GSM atakutana na Nabi kumpa mpango wao ujao ndani ya Yanga ikiwa ni sharti ambalo kocha huyo alitaka kulifahamu baada ya kikosi hicho kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mtihani mkubwa kwa GSM ni kupambana na Wasauzi Kaizer Chiefs ambao Mwanaspoti linafahamu kuwa ndio klabu ambayo inaongoza vita ya kumchukua kocha huyo raia wa Tunisia na amewaambia baadhi ya mastaa kuhusu dili hilo.
Juzi Nabi baada ya kuiwezesha Yanga kuchukua taji lake tano baada ya kushinda Fainali ya Kombe la ASFC alionekana kama anawaaga mashabiki wa timu yake mara baada ya kuwachapa Azam kwa bao 1-0, alikuwa akiwapungia mikono kwa ishara ya kuwaaga akiwa na mwanaye Hedi Nabi katika Uwanja wa CCM Mkwakwani akizunguka majukwaa ya mashabiki wa klabu hiyo jambo ambalo lilizua maneno.
MENEJA WA NABI
Jana Mwanaspoti lilimsaka mtoto wa Nabi, Hedi ambaye alisema bado baba yake hajafanya maamuzi ya mwisho na kwamba wakati wowote atakutana na uongozi wa klabu hiyo na kumalizana nao katika kujulikana kwa mustakabali.
"Siwezi kusema anaondoka wala anabaki kwasasa,b baba yangu ni mtu anayeheshimu viongozi mashabiki na hata wachezaji wake lakini kitu ambacho kitakwenda kutoa picha halisi ya baadaye ni pale atakapokutana na uongozi wa klabu yake," alisema Hedi.