Azam FC imetoa msamaha kwa wachezaji wake watatu ambao walikuwa wamefungiwa kutokana na kile ambacho walikisema ni utovu wa nidhamu kwa wachezaji hao lakini mchezaji mmoja amesema hapana.
Wachezaji ambao walifungiwa kwa zaidi ya wiki nne ni Mudathiri Yahya, Agrey Morris na Abubakar Salum “Sure Boy” ambapo msamaha huo ulitolewa wiki iliyopita lakini wachezaji hao hawakuweza kujiunga na timu kutokana na timu hiyo kuwa kwenye mpango wa mechi ya Mbeya City.
Baada ya mechi hiyo, wachezaji wawili Mdathiri Yahya na Agrey Morris wamejiunga tayari na wenzao lakini Abubakar Salum hajajiunga na timu hiyo kwa kile ambacho Afisa Habari wa klabu hiyo Thabit Zakaria “Zaka Zakazi” amekieleza kuwa mchezaji huyo ameomba kwa mdomo kuondoka klabuni hapo.
Zaka Zakazi amesema baada ya kuomba kuondoka kwa mdomo klabu imemwambia aandike barua (ombi la maandishi).
Taarifa za kuomba kuondoka kwa Sure Boy zinakuja kipindi ambacho mchezaji huyo amekuwa akihusishwa kujiunga na Yanga.