Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Morocco aifagilia Stars, Bitegeko aitwa kikosini

Hemed Morocco Kocha Morocco aifagilia Stars, Bitegeko aitwa kikosini

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kutoka suluhu dhidi ya wenyeji, Indonesia, Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Hemed Morocco, amewamwagia sifa vijana wake, akisema wameitendea haki mechi hiyo ya kirafiki iliyochezwa jijini Jakarta juzi mchana.

Stars imetumia mechi hiyo ya kirafiki kujiandaa kuikabili Zambia (Chipolopolo), katika mchezo wa Kundi E wa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026.

Morocco aliliambia Nipashe ameanza kuona mwanga katika kikosi chake kuelekea mechi ijayo dhidi ya Chipolopolo.

Kocha huyo alisema timu yake ilitawala vipindi vyote viwili na kutengeneza nafasi nyingi, ingawa hawakuzitumia vyema, lakini inaonyesha ni jinsi gani walivyopambana na kushika mafunzo aliyowapatia.

"Ilikuwa mechi nzuri, tuliwapa nafasi vijana wengi, imekuwa vizuri kwangu mimi kwa sababu sasa nitapata machaguo mengi na kikosi kipana.

Katika mechi hii tumecheza vizuri vipindi vyote viwili, tumetawala mchezo, tumezuia presha za wapinzani wetu, tumetengeneza nafasi nyingi, hilo kwangu ni jambo la msingi sana kuliko mengine," alisema kocha huyo.

Aliongeza atayafanyia kazi haraka mapungufu machache aliyoyaona ili kuhakikisha wanakuwa imara kabla ya kukutana na Zambia ambayo pia ina kikosi imara.

"Tunatakiwa turudi tena katika ubao wa mazoezi, tutaenda kutatua matatizo ambayo yameonekana, mechi hii imetusaidia kuangalia mapungufu kabla ya kuwavaa Zambia, hawa waliopo na tukichanganyika na wale ambao hawakuwapo, tutakuwa imara zaidi kwa kuwakabili wapinzani wetu," Morocco aliongeza.

Wakati huo huo, Morocco amemwongeza, Alphonce Bitegeko wa Azam FC katika kikosi chake. Mbali na Zambia, timu nyingine zilizoko katika Kundi E ni pamoja na vinara Morocco na Niger.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live