Baada ya Kituo cha Moro Kids kuingia mkataba wa makubaliano na ushirikiano na Yanga Sc Mwenyekiti wa kituo hicho, Idefonce Magale amesema mkataba huo utaenda kuwapa nguvu ya kuzalisha vijana wengi zaidi.
Magale amesema ni mafanikio makubwa kwao kuungana na Yanga SC katika jambo hilo.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu kuona tumeungana na Yanga SC. Ujio wao utakuwa maradufu na tunawashukuru sana.
“Tanzania kuna vituo vingi vya soka na kitendo cha Yanga SC kuja kwetu inamaanisha kuwa kimeongeza kitu kizuri kwetu.
“Tunaamini uwepo wao tutaenda kutoa wachezaji wengine mahiri wa kuitumikia Yanga SC watakaopata kipaumbele pamoja na mpira wa Tanzania” alisema Magale.
Miongoni mwa wachezaji wa Yanga SC waliowahi kupita katika kikosi hicho ni Abuutwalib Mshery, Dickson Job, Nickson Kibabage, Zawadi Mauya na Kibwana Shomari.
Ofisa Habari wa timu hiyo Ali Kamwe amesema wameamua kufanya hivyo ili kuifupisha safari ya kijana wa Kitanzania. Kamwe alisema uwepo wa ushirikiano wao na Moro Kids utakuwa na faida kwao na kituo hicho.